Lugha Nyingine
Utalii wa kimataifa kuimarika kikamilifu kwa kiwango cha kabla ya janga la COVID kufikia mwisho wa mwaka
MADRID - Huku watalii wapatao bilioni 1.1 wakiwa wamesafiri kimataifa katika miezi tisa ya kwanza ya Mwaka 2024, utalii wa kimataifa umefikia asilimia 98 ya kiwango cha kabla ya kuzuka kwa janga la COVID-19 mwaka 2019, takwimu za shirika la utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) zimeonyesha.
Katika ripoti yake ya Hali ya Utalii (Tourism Barometer) iliyotolewa jana Jumatano, shirika hilo lenye makao yake mjini Madrid, Hispania limekadiria kuwa sekta ya utalii "itaimarika kikamilifu" kufikia mwisho wa mwaka huu.
Kuongezeka kwa idadi ya watalii wa kimataifa kulisababishwa na mahitaji makubwa ya baada ya janga la COVID-19 barani Ulaya na ufanisi thabiti kutoka kwa masoko yenye vyanzo vikubwa vya watalii duniani, vile vile kuendelea kuimarika kwa maeneo ya vivutio vya utalii katika Asia Pasifiki.
Kuongezeka kwa watalii wanaowasili kumekuwa dhahiri sana katika nchi za Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika, ambazo zimezidi kiwango cha Mwaka 2019, zikiwa na ongezeko la asilimia 29, asilimia 1 na asilimia 6 mtawalia.
Watalii wa kimataifa wanaowasili katika eneo la Asia-Pasifiki walifikia asilimia 85 ya mwaka 2019 hadi kufikia Septemba 2024, ikionyesha maendeleo makubwa kutoka asilimia 66 ya mwaka 2023. Nchi za Amerika zimefikia asilimia 97 ya kiwango cha 2019.
Ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa wanaowasili limeenda sambambma na ongezeko la mapato yanayotokana na utalii katika robo tatu za kwanza za mwaka 2024.
Nchi 35 kati ya 43 zilizo na takwimu zinazopatikana kuhusu upokeaji wa watalii zimezidi kiwango cha kabla ya janga katika miezi minane hadi tisa ya kwanza ya mwaka 2024, huku nyingi zao zikiripoti ukuaji wa tarakimu mbili ikilinganishwa na mwaka 2019.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Utalii Zurab Pololikashvili amesema; "Ukuaji mkubwa unaoonekana katika upokeaji wa watalii ni habari njema kwa uchumi kote duniani."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma