

Lugha Nyingine
Wapalestina takriban 20 wauawa katika shambulizi la Israel Kusini mwa Gaza
GAZA - Wapalestina takriban 20 wameuawa siku ya Jumatano katika shambulizi la Israel lililolenga makazi ya kujihifadhi ya watu waliokimbia makazi yao magharibi mwa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza, ambapo vyanzo vya habari na mashuhuda wa Palestina wamesema kwamba ndege za kivita za Israeli zililenga makazi hayo, ambayo yanahifadhi watu waliolazimika kukimbia makazi yao katika eneo la Mawasi, kwa kurusha angalau kombora moja.
Wakati huo huo, Shirika la Ulinzi wa Kiraia la Palestina mjini Gaza imetoa taarifa kwa vyombo vya habari ikisema timu yake inafanya kazi ya kuzima moto uliozuka kwenye mahema kufuatia shambulizi hilo la Israel.
Madaktari wameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba vikundi vya uokoaji vimepata miili ya watu wasiopungua 20, wakiwemo watoto watano, na kusafirisha makumi ya majeruhi kuwapeleka hospitalini.
Jeshi la Israel bado halijatoa maoni yoyote kuhusu shambulizi hilo.
Israel imekuwa ikianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza kulipiza kisasi dhidi ya uvamizi wa Hamas kupitia mpaka wa kusini mwa Israel Oktoba 7, 2023, ambapo watu takriban 1,200 waliuawa na wengine karibu 250 kuchukuliwa mateka.
Idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Israel mjini Gaza imeongezeka hadi 44,532, mamlaka za afya za Gaza zimesema katika taarifa siku ya Jumatano.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma