

Lugha Nyingine
Jeshi la Israeli ladhibiti maeneo ya mpaka, na kushambulia silaha za kimkakati nchini Syria
![]() |
Picha hii ilipigwa Desemba 8, 2024 ikionyesha wanajeshi wa Israel karibu na eneo la kutenganisha mapigano kati ya Syria na Israel katika Milima ya Golan. (Ayal Margolin/JINI kupitia Xinhua) |
DAMASCUS/JERUSALEM - Jeshi la Israel limechukua udhibiti wa maeneo karibu na mpaka wa Israel na Syria na kushambulia silaha za kimkakati nchini Syria kufikia Jumatatu, kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Syria na Israel.
Siku ya Jumatatu, vifaru vya Israel viliingia katika mji wa kusini-magharibi mwa Syria, Quneitra karibu na Milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu, vikifikia jengo la utawala wa jimbo huku droni zikizunguka angani, chanzo cha habari nchini Syria kimeliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria, shirika la kufuatilia vita la Uingereza, limesema maeneo mengi ya Quneitra yameshambuliwa.
Mjini Damascus, mwandishi wa habari wa Xinhua alishuhudia ndege za kivita za Israel zikiruka angani. Makundi ya watu waliokuwa wakinyoosha juu silaha zilizoibiwa kutoka kwenye vituo vilivyotelekezwa vya jeshi wakizunguka-zunguka katika mitaa iliyokuwa imejaa vioo vilivyopasuliwa, magari ya kijeshi yaliyoharibiwa, benki zilizoporwa mali, magari yaliyoibiwa, na vioski vilivyovamiwa.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Sa'ar amesema Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari kwamba wanamgambo nchini Syria walivuka eneo la kutenganisha mapigano kati ya Syria na Israel wikiendi iliyopita, wakikiuka makubaliano ya kusimamisha vita kati ya nchi hizo mbili.
Wanamgambo hao pia walishambulia maeneo ya Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Uangalizi wa Usimamishaji wa Mapigano, ambacho kinafuatilia makubaliano hayo karibu na mpaka, Sa'ar amesema.
"Katika kulipiza, na kutokana na tishio kwa jamii zetu katika Milima ya Golan, IDF (Vikosi vya Ulinzi vya Israel) vilifanya operesheni lengwa na ya muda mfupi ili kudhibiti maeneo hayo karibu na mpaka," amesema.
Katika taarifa yake kwenye video iliyotolewa na ofisi yake siku ya Jumapili, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema ameamuru wanajeshi kuchukua udhibiti wa maeneo hayo kwa muda ili kuhakikisha hayaangukii mikononi mwa makundi ya wapiganaji yanayoongozwa na Hayat Tahrir al-Sham ambaye mashambulizi yake makubwa kote Syria tangu Novemba 27 yamesababisha kuanguka kwa haraka kwa serikali ya Rais Bashar al-Assad siku ya Jumapili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma