

Lugha Nyingine
Mkulima wa pilipili wa Rwanda akifanyia mageuzi kilimo kwa utaalamu, maono na biashara ya China
KIGALI - Herman Uwizeyimana, mkulima wa pilipili nchini Rwanda mwenye Shahada ya Uzamivu ya Ikolojia kutoka Akademia ya Sayansi ya China, alifanya uamuzi wa kijasiri mwaka 2019 kuacha kazi yake ya utumishi wa umma na kuanza kazi ya ukulima.
Licha ya changamoto za kukosa mshahara wa kawaida wa kila mwezi, aliona kilimo kama fursa ya kuleta matokeo halisi kwa maisha ya Wanyarwanda na kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Uwizeyimana aliingia katika kilimo cha pilipili chini ya Fisher Global, kampuni ya kilimo ya Rwanda inayojihusisha na ukuzaji na uuzaji nje wa pilipili. Anaiona biashara kati ya China na Rwanda kuwa ni baraka, na tabasamu lake la kila siku ni uthibitisho wa mafanikio yake kama mmoja wa wakulima wanaouza nje mazao yao kwenye soko la nchi hiyo ya Asia.
Akiwa mtaalam wa ikolojia, ujuzi wake wa Uwizeyimana umekuwa muhimu katika kuendesha biashara ya kilimo yenye mafanikio ambayo imetoa ajira kwa mamia ya Wanyarwanda wenyeji.
Akikumbusha muda wake wa kusoma nchini China, Uwizeyimana ametimiza ndoto yake ya kutoa mchango kwa maendeleo ya Rwanda kupitia biashara ambayo inanufaisha jamii za wenyeji.
"Tunafanya kazi na wakulima karibu 1,500. Tunatoa mbegu, msaada wa kiufundi, wataalamu wa kilimo na mafunzo sahihi. Baada ya kuvuna, tunakausha pilipili kabla ya kuiuza China," Uwizeyimana ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano ya hivi karibuni.
Cassien Habineza, mtaalamu mkuu wa kilimo wa kampuni hiyo, alijiunga na timu hiyo mwaka 2023. Ameeleza mengi aliyojifunza, ambayo yamemnufaisha binafsi na kitaaluma. “Pamoja na mapato yenye uhakika, nimeweza kuboresha hali ya kiuchumi ya familia yangu,” amesema.
Fisher Global inaendesha mashamba ya pilipili kwenye hekta 300 kote nchini Rwanda, ikifanya kazi na jumuiya mbalimbali za ushirika wa kilimo. Ingawa kampuni hiyo inajikita katika kilimo cha pilipili, pia inalima maharagwe ya soya na mahindi, huku maharagwe hayo ya soya yakitumika kama zao la mzunguko kudumisha rutuba ya udongo.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Fisher Global imeuza nje kati ya tani 200 na 300 za pilipili kavu kwa mwaka, huku tani 230 zikiuzwa nje mwaka jana pekee. Lengo la Uwizeyimana, hata hivyo, ni kupanua mauzo ya nje hadi kufikia tani 1,500 za pilipili kavu kwa mwaka.
Uwizeyimana ameonyesha matumaini kuhusu sera mpya ya China, ambayo, itaanza kutumika Desemba 1, inatoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa bidhaa kutoka nchi zilizoendelea ambazo zina uhusiano wa kidiplomasia nayo. Anaona sera hiyo ni hamasa kubwa kwa wakulima wa Afrika na anakadiria kuwa itaongeza kiasi cha mauzo ya nje ya bidhaa za Afrika nchini China. "Sera hii inaonyesha kuwa China ni rafiki mzuri wa nchi za Afrika," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma