Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu atoa ushahidi katika kesi ya ufisadi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 11, 2024
Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu atoa ushahidi katika kesi ya ufisadi
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akionekana katika mahakama ya Tel Aviv, Israel, Desemba 10, 2024. (Reuven Kastro/JINI kupitia Xinhua)

JERUSALEM - Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametoa ushahidi kwa mara ya kwanza jana Jumanne katika kesi yake ya muda mrefu ya ufisadi, ikiashiria wakati muhimu wa kesi hiyo katika kipindi ambacho anasimamia vita katika Ukanda wa Gaza na anakabiliwa na hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.

Netanyahu anakabiliwa na mashtaka ya rushwa, ulaghai na uvunjaji wa uaminifu. Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani zaidi ya miaka mitano iliyopita, anatuhumiwa kuwezesha kanuni zenye upendeleo kwa kampuni kubwa ya mawasiliano ya simu ili kutangazwa vizuri na vyombo vya habari kuhusu yeye na familia yake. Pia anadaiwa kupokea zawadi za kifahari, zikiwemo sigara kubwa na shampeni zenye thamani ya maelfu ya dola, kutoka kwa mzalishaji maudhui wa Hollywood kwa ajili ya kumsaidia katika masuala ya kibinafsi.

Netanyahu alifika katika mahakama hiyo ya Tel Aviv majira ya saa 4 Asubuhi kwa saa za huko ambapo alikutana na waandamanaji na waungaji mkono. Baadhi walionyesha kumuunga mkono, huku wengine wakimtaka aongeze juhudi za kuachiliwa kwa mateka takriban 100 ambao bado wanashikiliwa Gaza.

Mawaziri na wabunge wa muungano wa vyama vinavyounda serikali anayoiongoza, wakiitikia wito kutoka kwa ofisi ya Netanyahu usiku wa kuamkia siku ya kesi hiyo, pia walihudhuria ili kuonyesha kumunga mkono.

Wakati wa kuanza kwa usikilizaji wa shauri hilo, mwanasheria wa Netanyahu, Amit Hadad, alikosoa mfumo wa mahakama wa Israel, akiita kesi hiyo "mashtaka ya kisiasa." Hadad amelielezea shitaka hilo kuwa "lenye dosari na batili" na akajenga hoja kwamba kesi hiyo inapaswa kutupiliwa mbali.

Netanyahu alianza kuwasilisha ushahidi wake majira ya takriban saa 5:30 asubuhi, akianza kwa kauli ya, "Nimekuwa nikisubiria miaka minane kwa wakati huu ili kusema ukweli kama ninavyoukumbuka." Ameuelezea ushahidi wake kama "fursa ya kutoboa shutuma zisizo na msingi" dhidi yake.

Netanyahu, ambaye amekuwa waziri mkuu wa Israel kwa miaka zaidi ya 17, anashikilia rekodi ya kuwa kiongozi wa muda mrefu zaidi wa nchi hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha