DRC yaripoti visa karibu 54,000 vinavyoshukiwa kuwa vya ugonjwa wa mpox mwaka huu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 13, 2024
DRC yaripoti visa karibu 54,000 vinavyoshukiwa kuwa vya ugonjwa wa mpox mwaka huu
Wakaazi wenyeji wakinawa mikono kwenye kampeni ya kujenga uelewa dhidi ya ugonjwa wa mpox mjini Goma, Jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Desemba 12, 2024. (Picha na Zanem Nety Zaidi/Xinhua)

KINSHASA - Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeripoti visa 53,860 vinavyoshukiwa kuwa vya ugonjwa wa mpox, ikiwa ni pamoja na vifo 1,225, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, Wizara ya Afya ya Umma ya nchi hiyo imetangaza siku ya Alhamisi ambapo mamlaka hiyo ya afya imesema kuwa asilimia karibu 30 ya visa hivyo vimerekodiwa Kivu Kusini, jimbo la mashariki la nchi hiyo lililoathiriwa zaidi.

Kama eneo kuu lililiathiriwa zaidi, DRC inakabiliwa na changamoto kubwa katika ufuatiliaji na upimaji, hasa katika ngazi ya majimbo. Vikwazo hivyo vinazuia kugunduliwa kwa visa na kucheleweshwa kwa juhudi za mwitikio, vikidhoofisha uwezo wa nchi hiyo wa kudhibiti janga hilo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya katika ripoti yake mpya iliyotolewa Jumanne.

Katika kampeni ya chanjo iliyozinduliwa Oktoba 6, watu zaidi ya 51,600 wamechanjwa katika majimbo sita, kwa mujibu wa WHO. Hata hivyo, Waziri wa Afya wa DRC Roger Kamba amesema kuwa nchi hiyo inahitaji dozi takriban milioni tatu za chanjo kuhudumia watu milioni 2.5.

WHO imesisitiza kwamba kuibuka tena kwa virusi vya mpox bado ni dharura ya afya ya umma inayofuatiliwa kimataifa. Mwezi Agosti, shirika hilo lilitangaza dharura ya kiafya huku janga hilo likienea kote barani Afrika, likiwa limeathiri nchi 19 za bara hilo hadi sasa.

Ugonjwa wa Mpox, ambao pia unajulikana kwa jina la monkeypox, uligunduliwa kwa mara ya kwanza katika nyani wa maabara mwaka 1958. Ni ugonjwa wa nadra wa kuenezwa kwa kasi na virusi ambao kwa kawaida huambukizwa kupitia maji maji ya mwili, matone ya kupumua, na nyenzo zilizoambukizwa. Maambukizi kwa kawaida husababisha homa, vipele, na kuvimba kwa nodi za limfu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha