

Lugha Nyingine
Kituo cha kwanza cha uvumbuzi cha chuo kikuu chazinduliwa nchini Botswana
GABORONE - Botswana imezindua Kituo chake cha kwanza cha Uvumbuzi cha Chuo Kikuu (UniPod) siku ya Jumatatu, kikiwa na lengo la kuwawezesha vijana, kuhimiza uvumbuzi na kugeuza mawazo yenye uvumbuzi kuwa suluhu halisi na zinazoweza kuuzwa.
Mpango huo ni ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Botswana, Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia, na Wizara ya Elimu ya Juu ya Botswana. Baada ya kuandaa kwa miezi kadhaa, kituo hicho kinatarajiwa kuhimiza maendeleo ya kiuchumi ya Botswana kwa kuziba pengo kati ya elimu ya juu na viwanda.
Ikiwa na nafasi za kubuni na kuunda mambo mapya, maabara za uundaji, nafasi za kufanya kazi pamoja na studio za kibunifu, kituo hicho kinatoa zana na rasilimali hitajika ili kuendeleza uvumbuzi. Kwa kuwa na teknolojia za hali ya juu kama vile vichapishaji vya 3D, vikata leza na nyenzo za kuunda, wavumbuzi wataweza kufanya majaribio, kuunda na kuboresha mawazo yao. UNDP imewekeza dola za Kimarekani takriban milioni 1.4 katika mpango huo.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo hicho iliyofanyika Gaborone, mji mkuu wa Botswana, Ahunna Eziakonwa, katibu mkuu msaidizi ambaye pia ni mkurugenzi wa UNDP Kanda ya Afrika, amesema kuwa UniPod itasaidia wajasiriamali wa Afrika katika kutoa fursa za ajira na kushughulikia masuala ambayo jamii za Afrika zinakabiliana nayo, kama vile mabadiliko ya tabianchi.
Justin Hunyepa, Naibu Waziri wa Elimu ya Juu wa Botswana, amesema kituo hicho kitawapa watu wa Botswana mawazo na dhana ili kupata vifaa vya kisasa, majaribio, miundo na soko. Amesema mpango huo unaendana na maono ya Botswana ya kuwa uchumi unaoendeshwa na maarifa na uvumbuzi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma