

Lugha Nyingine
Ripoti yaonyesha kampuni za China zinahimiza ukuaji wa kijani, ujenzi wa mambo ya kisasa nchini Kenya
![]() |
Hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya Uwajibikaji wa Kijamii wa Kampuni za China nchini Kenya ikifanyika Nairobi, Kenya, Desemba 17, 2024. (Xinhua/Li Yahui) |
NAIROBI - Kenya imepata mafanikio katika maendeleo ya kijani, ujenzi wa mambo ya kisasa na uboreshaji wa ujuzi,kutokana na ushiriki wa kampuni za China nchini humo, kwa mujibu wa ripoti ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) iliyozinduliwa Jumanne mjini Nairobi.
Toleo la nne la ripoti hiyo iliyoandaliwa na Shirikisho la Uchumi na Biashara la China nchini Kenya (KCETA) ikihusisha mwaka 2022-2023, imesema kuwa kampuni hizo zimeunga mkono ajenda ya muda mrefu ya ukuaji na mageuzi ya Kenya.
Uzinduzi wa ripoti hiyo uliopewa kaulimbiu ya “Kushirikiana Kuendeleza Ujenzi wa Mambo ya Kisasa na Kujenga Jumuiya yenye Mustakabali wa Pamoja,” ulihudhuriwa na viongozi waandamizi, wanadiplomasia na watendaji wa sekta hiyo.
Mohamed Daghar, katibu mkuu katika Wizara ya Barabara na Uchukuzi ya Kenya, amesema ripoti hiyo imesisitiza mchango mkubwa wa kampuni za China katika ujenzi wa mambo ya kisasa wa Kenya kupitia maendeleo ya miundombinu, ujuzi na uhamishaji wa teknolojia, utoaji wa fursa za ajira na mawasiano ya kitamaduni.
"Tuko hapa ili kuthibitisha nguvu ya ushirikiano kati ya kampuni za China na serikali ya Kenya. Ushirikiano wetu unahusu miundombinu, TEHAMA, maji, ulinzi na elimu," Daghar amesema.
Kampuni wanachama 104 zinazowakilishwa na KCETA zimeunda njia mpya za ukuaji jumuishi wa Kenya, zikiingiza mtaji, ujuzi na teknolojia katika uchumi wa nchi hiyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CSR.
Wakenya zaidi ya 60,000 waliajiriwa na kampuni hizo katika kipindi cha 2022-2023, huku kiwango cha wafanyakazi wenyeji kimezidi asilimia 90, ripoti hiyo imebaini.
Baadhi ya miradi mikuu iliyotajwa kwenye ripoti hiyo ambayo yameleta mageuzi katika maisha ya jamii za wenyeji ni pamoja na Reli ya SGR ya Mombasa-Nairobi, Shindano la Teknolojia la Afrika (Africa Tech Challenge), programu ya Huawei ya ujuzi wa kidijitali, Barabara Kuu ya Nairobi, Kituo cha Kuzalisha Umeme wa Megawati 50 kwa Jua cha Garissa kaskazini mashariki mwa Kenya na Bwawa la matumizi mbalimbali la Thwake kusini mashariki mwa Kenya.
Liu Chenghui, mwenyekiti wa KCETA ambaye pia ni naibu meneja mkuu wa Shirika la Barabara na Madaraja la China Makao Makuu ya Kenya, amesema kwamba kwa kuongozwa na moyo wa ushirikiano na urafiki, kampuni hizo za China nchini Kenya zinahimiza ustawishaji wa viwanda nchini humo.
"Tunahimiza kampuni zetu wanachama kuweka uwiano kati ya uwajibikaji wa kijamii na ulinzi wa mazingira na mambo ya kiuchumi," Liu amesema.
Zhou Zhencheng, balozi mdogo wa China nchini Kenya, amesema kuwa nchi zote mbili kwa pamoja zinahimiza ushirikiano wa kiwango cha juu katika Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, kama inavyodhihirishwa na miradi ya kuboresha maisha ya watu na miradi alama ya kitaifa ambayo imetekelezwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma