China na Malaysia zasaini makubaliano ya  ukarabati wa mradi mkubwa wa reli ya ECRL

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 19, 2024
China na Malaysia zasaini makubaliano ya  ukarabati wa mradi mkubwa wa reli ya ECRL
Waziri wa Uchukuzi wa Malaysia Anthony Loke Siew Fook (katikati) na Balozi wa China nchini Malaysia Ouyang Yujing (wa pili kulia) wakihudhuria hafla ya kutia saini makubaliano ya ubia kati ya Kampuni ya Ujenzi wa Mawasiliano ya China (CCCC) na Kampuni ya reli ya Malaysia (MRL) mjini Putrajaya, Malaysia, Desemba 18, 2024. (Picha na Chong Voon Chung/Xinhua)

PUTRAJAYA, Malaysia - Kampuni ya Ujenzi wa Mawasiliano ya China (CCCC), inayojenga mradi mkubwa wa reli ya pwani ya mashariki (ECRL) nchini Malaysia, imetia saini makubaliano jana Jumatano ya kuanzisha kampuni ya uendeshaji na ukarabati kwa pamoja na Kampuni ya reli ya Malaysia (MRL), ambayo ni Mmiliki wa mradi huo wa ECRL.

Hafla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo ya ubia kati ya MRL na CCCC kwa ajili ya uendeshaji na ukarabati wa reli hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Uchukuzi wa Malaysia Anthony Loke Siew Fook na Balozi wa China nchini Malaysia Ouyang Yujing.

Loke amesema makubaliano hayo yataruhusu pande zote mbili kuchangia gharama za uendeshaji wa ECRL, vilevile kuwezesha ujuzi wa kiufundi na utaalamu, huku matokeo ya mwisho yakiwa ni kuleta faida ya maendeleo ya pamoja inayoletwa na mradi huo.

“Makubaliano hayo yanaweza kusukuma maendeleo ya miundombinu ya nchi hiyo katika kuimarisha huduma za usafiri za kisasa, zenye ufanisi na rafiki kwa mazingiraili kunufaisha wananchi na kuongeza nguvu za ushindani wa kiuchumi wa nchi,” amesema katika hotuba yake kwenye hafla hiyo.

"Mtandao wa ECRL wenye urefu wa kilomita 665 una mchango muhimu katika kuunganisha majimbo ya Pwani ya Mashariki na Bonde la Klang, hivyo kuongeza mawasiliano ya watu na kuwezesha uwezo wa watu wenye ujuzi katika sekta ya reli," amesema.

Kwa upande wake, Balozi Ouyang Yujing amesema kuwa ECRL ambayo imezingatiwa sanana nchi zote mbili, itakuwa na mchango muhimu katika kuhimiza maendeleo, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya watu, na kuingiza msukumo mpya katika maendeleo ya uchumi wa kikanda.

Pia ameelezea matumaini kwamba pande zote mbili zitafanya kazi kwa bidii ili kutunza na kuendesha reli hiyo vizuri, kuboresha kila wakati faida zake za kiuchumi na kijamii, na kuifanya kuwa njia ya utajiri na furaha kwa umma.

ECRL inaanzia kutoka kitovu kikubwa zaidi cha usafiri cha Malaysia cha Bandari ya Klang na kuvuka peninsula hadi Jimbo la Kelantan kaskazini mashariki. Inatarajiwa kuimarisha kwa kiasi kikubwa muunganisho na kuleta ukuaji wenye uwiano zaidi kwa nchi hiyo ya Asia Kusini-Mashariki kwa kuunganisha eneo lake ambalo halijaendelea kwenye pwani ya mashariki na kitovu cha kiuchumi katika pwani ya magharibi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha