Kilimo cha kahawa chatoa maisha kwa watu katika eneo la kati la Kenya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 23, 2024
Kilimo cha kahawa chatoa maisha kwa watu katika eneo la kati la Kenya
Mkulima akichuma mbegu za kahawa katika shamba la kahawa mjini Kirinyaga, Kenya, Desemba 20, 2024. (Xinhua/Wang Guansen)

NAIROBI - Ilikuwa ndiyo kupita saa sita mchana wakati Richard Muthie alipokuwa amesimama kwenye mlango wa kiwanda cha kahawa cha Ushirika wa Wakulima wa Mutira, yuko tayari kuwasilisha mavuno yake. Zilizokuwa pamoja na mkulima huyo mwenye umri wa miaka 50 ni mbegu nyuekundu zilizoiva za kahawa zenye uzito wa kilo 30 ambazo zilikuwa zimechunwa naye punde zikiwa freshi asubuhi hiyo.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, Muthie amewasilisha kilo 400 za mbegu za kahawa kwa ajili ya kusindika katika kinu cha ushirika huo, kilichoko umbali wa takriban kilomita nne kutoka shamba lake la nusu ekari katika kaunti ya kati ya Kenya ya Kirinyaga. Ardhi hiyo aliyorithi kutoka kwa baba yake imekuwa chanzo cha maisha yake. "Kahawa hunipa mapato kukidhi mahitaji yangu ya nyumbani," Muthie amesema.

Muthie ni mmoja wa wakulima wadogo 8,000 ambao kwa pamoja wanamiliki Ushirika wa Wakulima wa Mutira. Wanatoa jukumu muhimu katika shughuli za ushirika, ambazo zinaingiliana sana na kilimo cha eneo hilo.

Martin Kinyua, katibu wa ushirika huo, amesema kuwa msimu wa kuvuna kahawa huanza Oktoba na kwa kawaida hukamilika mwishoni mwa mwaka. Kisha wakulima husubiri msimu mrefu wa mvua, unaotarajiwa Machi 2025, kwa mavuno yajayo kwani mazao yao yanategemea sana mvua.

Mwaka 2023, ushirika huo ulisindika mbegu za kahawa zenye uzito wa takriban kilo milioni 4.88 kutoka kwa wanachama wake. Sehemu kubwa ya mazao ya ushirika huo yalikuwa yamesindikwa kwa nusu na kuuzwa kwa wingi katika Soko la Kahawa la Nairobi. Hata hivyo, ni asilimia moja tu iliyosindikwa kikamilifu na kuuzwa kama bidhaa ya mwisho kwa watumiaji wa ndani.

Ili kuongeza faida kwa wakulima, ushirika huo umeweka lengo kubwa la kusindika kikamilifu angalau asilimia tano ya kahawa yao na kuingia katika masoko ya ng'ambo, ikiwa ni pamoja na China.

Kinyua amesema kuwa mapato ya juu yamehimiza wakulima kupanua ardhi ya kulima kahawa, ambayo inatarajiwa kuongeza uwezo wa kiwanda cha kahawa mwaka huu.

Victor Munene, mtaalamu wa kilimo katika ushirika huo, amesisitiza uwezekano mkubwa wa faida ya kilimo cha kahawa katika eneo hilo. "Kipande cha nusu ekari ya ardhi kinaweza kuleta faidatakriban shilingi 96,000 za Kenya (dola za Kimarekani kama 742) katika mapato ya kila mwaka," Munene amesema.

Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Kenya zinaonyesha umuhimu wa sekta hiyo. Mwaka 2023, uzalishaji wa kahawa nchini humo ulifikia tani 48,648, ukizalisha dola za Kimarekani takriban milioni 251.86 katika mauzo ya nje. Kahawa inaendelea kuwa miongoni mwa mambo yanayoingiza fedha nyingi za kigeni nchini Kenya, pamoja na chai na kilimo cha bustani.

Kwa wakulima kama Kellen Wambui, kahawa ina maana ya maisha, badala ya mazao tu. Mama huyo wa watoto watatu mwenye umri wa miaka 50 amekuwa akipanda kahawa kwa miaka mitano. "Mwaka huu, nimefikisha kilo 500 za mbegu za kahawa kiwandani," amesema.

Mapato kutokana na kahawa yamemwezesha kulipa ada za shule za watoto wake na kukidhi mahitaji mengine ya nyumbani.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha