Reli mpya ya mwendo kasi yaimarisha muunganisho wa kundi la miji mikubwa ya mashariki mwa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 27, 2024
Reli mpya ya mwendo kasi yaimarisha muunganisho wa kundi la miji mikubwa ya mashariki mwa China
Treni ya mwendokasi kutoka stesheni ya Mji wa Huzhou hadi Stesheni ya Reli ya Hongqiao ya Shanghai, mashariki mwa China, Desemba 26, 2024. (Xinhua/Fang Zhe)

SHANGHAI - Reli mpya ya mwendo kasi imeanza kufanya kazi siku ya Alhamisi, ikiimarisha mtandao wa reli unaounganisha miji mikubwa katika eneo la Delta ya Mto Changjiang mashariki mwa China, ambalo ni eneo lenye nguvu kubwa za kiuchumi nchini China.

Reli hiyo ya mwendo kasi ya Shanghai-Suzhou-Huzhou yenye urefu wa kilomita 164 imesanifiwa kupitisha treni za kuendeshwa kwa kasi ya kilomita 350 kwa saa na kuwekwa kwa stesheni nane, inaunganisha Stesheni ya Hongqiao ya Shanghai na stesheni za Mji wa Suzhou wa Mkoa wa Jiangsu na Mji wa Huzhou wa Mkoa wa Zhejiang.

"Hii ni reli ya kwanza ya mwendo kasi inayounganisha vituo vitatu vikuu vya kiuchumi vya mikoa ya Jiangsu na Zhejiang na mji wa Shanghai kwenye Delta ya Mto Changjiang ," amesema Chen Guoquan, kutoka Shirika la Ujenzi wa Reli la China, ambalo ni msanifu wa mradi wa reli.

Kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo mpya, urefu wa mtandao wa reli unaoendeshwa katika eneo la Delta ya Mto Changjiang umepita kilomita 15,000, ambapo karibu nusu yake ni reli ya mwendo kasi.

"Kabla ya huduma hii mpya ya treni, usafiri kati ya Huzhou na Shanghai ulihitaji kuchukua saa mbili hivi. Sasa, unachukua dakika 43 tu," amesema Lou Li kutoka Shanghai, ambaye alisafiri na familia yake kwenda likizo huko Nanxun, ambao ni mji wa kihistoria wenye vivutio vya utalii katika Huzhou.

Kang Aiqi, meneja mkuu wa kampuni ya teknolojia za nyenzo mpya ya Suzhou amesema, alikuwa ametarajia kwa hamu kufunguliwa kwa reli hiyo ya mwendo kasi. "Reli hiyo itarahisisha sana usafiri kwa wafanyabiashara katika eneo hilo la delta."

Kwenye kando za reli hiyo, viwanda vya teknolojia ya hali ya juu vitaibuka kwa makundi, ambavyo vitaharakisha zaidi maendeleo ya sifa bora ya ukanda huo wa kiuchumi, Zhang Zhipeng, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Mawasiliano cha Shanghai amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha