

Lugha Nyingine
Mawaziri wa GCC watoa wito wa umoja wa Syria, na kulaani mashambulizi ya Israel
KUWAIT CITY - Baraza la Mawaziri la Baraza la Ushirikiano la Eneo la Ghuba (GCC) limezitaka pande mbalimbali nchini Syria "kuzingatia maslahi ya kitaifa" na kusisitiza kuunga mkono mamlaka ya Lebanon kwenye mkutano wake maalum wa 46 huko Kuwait, ambapo katika taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la Kuwait, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait Abdullah Ali Al-Yahya aliyeongoza mkutano huo, amesisitiza msimamo wa pamoja wa GCC kuhusu uhuru na mamlaka ya Syria, akikataa uingiliaji wa nje katika masuala ya Syria.
Al-Yahya amezitaka pande zote nchini Syria kuanza tena mchakato wa kisiasa, kushiriki katika mazungumzo jumuishi, na kupewa kipaumbele umoja wa kitaifa ili kurejesha amani na utulivu.
"Eneo la Mashariki ya Kati linakabiliwa na changamoto na migogoro inayokua kwa kasi, ambayo inahitaji kuimarishwa kwa juhudi na ushirikiano wa pamoja. Kufikia amani nchini Syria na Lebanon kutakuwa na athari chanya kwa usalama na utulivu wa nchi nyingine za Kiarabu," Al-Yahya amesema.
Baraza hilo limehimiza Syria kufanya mazungumzo ya pande zote ya kitaifa na kuidhinisha hatua za kulinda raia, kuharakisha maridhiano na kuzuia umiliki wa silaha.
Wameeleza kuunga mkono pendekezo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuanzisha ujumbe maalum wa kusaidia mchakato wa mpito wa Syria.
Mawaziri hao wamelaani vikali mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel dhidi ya Syria, hususan ukaliaji kimabavu wa Israel katika eneo la mpaka, wakiueleza kuwa ni "ukiukaji wa wazi" wa mamlaka ya Syria na Makubaliano ya Kutokupigana ya mwaka 1974.
Wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya hujuma hizo na kuhakikisha Israel inajiondoa katika maeneo yote ya Syria inayoyakalia kwa mabavu.
Kuhusu Lebanon, baraza hilo limesisitiza kuunga mkono mamlaka na utulivu wa nchi hiyo, likisisitiza ulazima wa kutekeleza mageuzi ya kina ya kisiasa na kiuchumi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma