

Lugha Nyingine
Kampuni za China zahimizwa kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya Zambia
LUSAKA – Kampuni za China nchini Zambia zinapaswa kuchukua nafasi ongozi katika kuendesha uvumbuzi wa nchi hiyo na kuendana na mabadiliko ya muundo wa teknolojia na viwanda duniani, Balozi wa China nchini Zambia Han Jing amesema kwenye mkutano wa mwaka na Baraza la biashara lililoandaliwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China nchini Zambia, mjini Lusaka.
"Nahimiza wafanyabiashara wa China kuchangamkia fursa zinazojitokeza nchini Zambia katika sekta kama vile nishati ya jua, uchimbaji madini usio na uchafuzi wa mazingira, TEHAMA, na magari yanayotumia umeme, huku wakipanua ushirikiano katika maendeleo ya kijani na uchumi wa kidijitali," Balozi Han amesema.
Hafla hiyo ilijumuisha utoaji wa vyeti kwa kampuni za China kwa kutambua mchango wao katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uwajibikaji bora wa kibiashara kwa jamii na uendelezaji wa ajira.
Balozi huyo ameipongeza Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China nchini Zambia kwa mchango wake mkubwa katika kuhimiza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.
Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zambia Chipoka Mulenga amesifu kampuni za China kwa kuwekeza katika kuongeza thamani kwa malighafi za nchi hiyo.
"Serikali yetu imejikita katika kuhamasisha kuongeza thamani kwa malighafi, na tunafurahi kwamba kampuni za China tayari zimeanza kuwekeza katika eneo hili," Mulenga amesema.
Amesema kuwa kampuni mbili za China zimeanzisha viwanda nchini Zambia ili kuzalisha kebo za umeme kutokana na shaba inayopatikana nchini humo.
"Zambia inajifunza kutoka China, ambayo imefanya juhudi kubwa kuhimiza kuongeza thamani kwa malighafi kama mkakati wa ukuaji wa uchumi," Mulenga ameongeza. "Tunashukuru kwamba kampuni za China zimeitikia wito wetu wa uwekezaji katika kuongeza thamani."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma