

Lugha Nyingine
Taasisi ya China yakabidhi matangi ya maji kwa jamii za vijijini za Ethiopia
ADDIS ABABA – Taasisi ya Maendeleo Vijijini ya China (CFRD), ambayo ni shirika la kijamii la China lenye dhamira ya kupunguza umaskini, imekabidhi matangi ya maji kwa jamii za vijijini katikati mwa Ethiopia siku ya Ijumaa.
Hafla maalum ilifanyika katika Shule ya Msingi ya Obaay nje kidogo ya Kitongoji cha Dukem, umbali wa kilomita takriban 33 mashariki mwa Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, ikionyesha kukamilika na kukabidhi rasmi matangi hayo 40 ya maji. Mpango huo uliotekelezwa kwa kushirikiana na Kundi la Kampuni za Ujenzi na Mambo ya Mashine la Xuzhou (XCMG), inalenga kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi katika maeneo ya vijijini.
Viongozi wa serikali za mitaa na wanajamii wametoa shukrani zao kwa vifaa hivyo vipya, wakiipongeza CFRD na washirika wake kwa msaada wao muhimu katika kutoa vyanzo vya maji safi.
"Wakati wawekezaji na mashirika mengi yanashirikiana na jamii, ushirikiano huu unatumika kama kielelezo kwa wengine, ukitoa matumaini na mustakabali mwema kwa wakazi, ikiwa ni pamoja na wanafunzi watoto," amesema Duguma Kena, mkuu wa utawala wa Wilaya ya Melka.
Mkurugenzi wa CFRD nchini Ethiopia Yin Qian amesema kukabidhi matangi hayo ya maji yanaonesha dhamira ya shirika hilo ya kuboresha maisha katika jamii za vijijini nchini Ethiopia.
Amesema tangu mwaka 2017, CFRD na XCMG zimekuwa zikishirikiana katika mradi huo wa matangi ya maji, ukinufaisha wakazi zaidi ya 12,000 wa vijijini. Ameeleza kuwa, matangi hayo ya maji yameundwa kwa kuzingatia uendelevu, kwa kutumia mbinu za ujenzi endelevu na rafiki kwa mazingira.
Mradi huo hadi sasa umekamilisha na kukabidhi matangi zaidi ya 200 ya maji, yakitoa maji safi na salama kwa jamii zilizo hatarini katika maeneo kame ya Ethiopia, Yin ameeleza.
Li Jingchen, mwakilishi wa XCMG nchini Ethiopia, amesema kampuni hiyo imedhamiria kuboresha maisha ya watu wa Ethiopia ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za uwajibikaji kwa jamii.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma