Watu 29 wauawa kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 03, 2025
Watu 29 wauawa kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza
Watu wakiwa wamekusanyika kwenye jengo lililobomolewa kwa shambulizi la bomu la Israel katikati mwa mji wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wa Khan Younis, Januari 2, 2025. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

GAZA - Wapalestina takriban 29 wameuawa katika mashambulizi ya mabomu ya Israel kaskazini na kusini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Alhamisi, ikiwa ni pamoja na mkuu wa polisi wa Gaza, vyanzo vya habari vya Palestina vimesema, huku Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA likisema hakuna mahali popote ambapo ni salama kwa raia wa Palestina katika ukanda huo.

Kwa mujibu wa Shirika rasmi la Habari la Palestina, WAFA watu wanane wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi la mabomu la Israel karibu na eneo la makutano ya Al- Ayoun na Al-Lababidi, magharibi mwa Gaza, na wengine wanne wameuawa kutokana na shambulizi la mabomu la Israel katika kambi ya Ufukweni ya kaskazini, magharibi mwa mji huo.

Katika Mji wa Khan Younis, watu sita wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na shambulizi la Israeli ambao ulilenga jengo katikati mwa sehemu ya kusini ya mji huo, WAFA imeripoti.

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema katika taarifa yake siku ya Alhamisi kwamba Kikosi cha Anga kilifanya shambulizi kutokana na taarifa za ujasusi dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika kituo cha udhibiti na kamandi ndani ya jengo la serikali ya mji wa Khan Younis katika eneo la huduma za kibinadamu.

Mapema siku hiyo, Wapalestina wasiopungua 11 waliuawa katika shambulizi la Israel dhidi ya mahema katika eneo la Mawasi, magharibi mwa Khan Younis, wizara ya mambo ya ndani inayoongozwa na Hamas imesema.

"Meja Jenerali Mahmoud Salah, mkurugenzi mkuu wa jeshi la polisi la Gaza, na Hassam Shahwan, afisa mwandamizi katika mamlaka ya mambo ya ndani ya Hamas, ni miongoni mwa waliofariki," wizara hiyo imefafanua.

Katika taarifa tofauti, IDF imesema kwamba usiku kucha, ilifanya shambulizi kwa mujibu wa taarifa za ujasusi dhidi ya eneo la huduma za kibinadamu mjini Khan Younis na kumuua mkuu wa Kikosi cha Usalama wa Ndani cha Hamas kusini mwa Ukanda wa Gaza, Hassam Shahwan.

Kufuatia mashambulizi hayo ya Israel kwenye maeneo tengwa ya huduma za kibinadamu, Philippe Lazzarini, kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada kwa wakimbizi wa Palestina, UNRWA, kwenye mtandao wa kijamii wa X siku hiyo ya Alhamisi amesema kuwa hakuna usalama kwa raia popote pale mjini Gaza, wakati ambapo zaidi ya asilimia 80 ya eneo la Gaza ikiwa chini ya amri ya Israel ya kuondolewa kwa watu.

"Hakuna eneo la kibinadamu achilia mbali 'eneo salama.'" Lazzarini ameandika huku akitoa wito wa kukomeshwa kwa amri potofu za kuondolewa kwa watu na mauaji hayo ya raia, akionya kuwa kila siku bila usimamishaji wa mapigano huleta maafa zaidi.

Israel imekuwa ikifanya mashambulizi makubwa dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza kulipiza kisasi dhidi ya uvamizi wa Hamas kupitia mpaka wa kusini wa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo watu takriban 1,200 waliuawa na wengine takriban 250 kuchukuliwa mateka.

Idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na mashambulizi hayo yanayoendelea ya Israel katika Ukanda wa Gaza imeongezeka hadi 45,581, mamlaka ya afya ya Gaza imesema katika taarifa siku ya Alhamisi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha