Misri yavunja rekodi kwa kupokea watalii milioni 15.7 mwaka 2024

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 03, 2025
Misri yavunja rekodi kwa kupokea watalii milioni 15.7 mwaka 2024
Watalii wakitembelea Sphinx katika eneo la kivutio cha watalii la Piramidi za Giza mjini Giza, Misri, Januari 2, 2025. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

CAIRO - Waziri Mkuu wa Misri Mostafa Madbouly amesema kwamba nchi hiyo ilipokea watalii milioni 15.7 mwaka 2024, idadi ambayo imevunja rekodi, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na baraza la mawaziri la Misri, huku akisema takwimu hiyo "inaleta matumaini," Madbouly amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari Jumatano katika mji mkuu mpya wa utawala wa Misri mashariki mwa Cairo kwamba "kama isingekuwa matukio yaliyotokea katika kanda hiyo, idadi ya watalii ingefikia milioni 18."

Madbouly ameelezea matumaini yake kwamba Misri itatimiza lengo la idadi ya watalii milioni 18 mwaka 2025, "hasa baada ya Jumba Kuu la Makumbusho la Misri kufunguliwa rasmi mwaka huu."

Kutokana na janga la COVID-19, idadi ya watalii nchini Misri ilipungua kwa kiasi kikubwa kutoka zaidi ya milioni 13 mwaka 2019 hadi milioni 3.7 mwaka 2020, kisha ikafufua hatua kwa hatua hadi milioni 8 mwaka 2021, milioni 11.7 mwaka 2022 na milioni 14.9 mwaka 2023, kwa mujibu wa takwimu rasmi.

Sekta ya utalii ni moja ya vyanzo vikuu vya fedha za kigeni nchini Misri, pamoja na mapato kutoka Mfereji wa Suez, mauzo ya bidhaa nje ya nchi na fedha zinazotumwa na raia wa Misri wanaoishi nje ya nchi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha