Mwili wa Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter wawasili katika mji mkuu, Washington, D.C.

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 08, 2025
Mwili wa Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter wawasili katika mji mkuu, Washington, D.C.
Gari la kubebea maiti ya rais lililobeba jeneza lenye mwili wa Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter likiondoka kwenye uwanja wa ndege wa Joint Base Andrews mjini Maryland, Marekani, Januari 7, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

WASHINGTON - Mwili wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Jimmy Carter, aliyeaga dunia hivi karibuni akiwa na umri wa miaka 100, umewasili Washington, D.C. jana Jumanne ambapo ndege ya rais iliyobeba mwili wake iliondoka Atlanta, Georgia, mapema siku hiyo asubuhi na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Joint Base Andrews mjini Maryland, nje kidogo ya mji mkuu huo, Jumanne alasiri.

Kisha jeneza lenye mwili wa Carter lilipakiwa kwenye gari la kubebea maiti ya rais na kusafirishwa hadi kwenye Jumba la Kumbukumbu la Kikosi cha Majini cha Jeshi la Marekani kwenye mtaa wa Pennsylvania, kabla ya kupelekwa kwenye Bunge la Marekani, Capitol Hill.

Ibada ya kumbukumbu imepangwa kufanyika katika Capitol Rotunda, huku hotuba za wasifu wa marehemu zikitolewa na Makamu wa Rais Kamala Harris, Kiongozi wa Wabunge walio Wengi katika Seneti John Thune na Spika wa Bunge Mike Johnson.

Familia ya Carter, vilevile maofisa kadhaa walio bado hai waliotumikia Baraza la Mawaziri la urais wa Carter, wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo.

Jeneza la Carter litawekwa katika Rotunda na litakuwa wazi kwa utazamaji wa umma kuanzia Jumanne baadaye (kwa saa za huko). Mwili wake utahifadhiwa hadi Alhamisi asubuhi, wakati ibada ya kumwombea itakapofanyika katika Kanisa Kuu la Kitaifa la Washington.

Rais wa Marekani Joe Biden hapo awali alitangaza Januari 9, 2025 kuwa Siku ya Kitaifa ya Maombolezo kote Marekani kwa ajili ya rais huyo wa zamani.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha