Lugha Nyingine
Wanaanga wa Chombo cha Shenzhou-18 wakutana na waandishi wa habari baada ya kurudi kutoka anga ya juu
BEIJING - Wanaanga watatu wa chombo cha Shenzhou-18 cha China wamekutana na waandishi wa habari jana Jumatano, hii ni mara ya kwanza kwao kukutana na umma tangu warudi kutoka anga ya juu miezi miwili iliyopita.
Wanaanga hao wote watatu -- Ye Guangfu, Li Cong na Li Guangsu -- wako katika hali nzuri ya kimwili na kiakili. Nguvu za misuli, ustahimilivu na uwezo wao wa moyo na mapafu wakati wa kufanya mazoezi kimsingi vimerejea katika viwango vya kabla ya kupaa kwenda anga ya juu.
China ilirusha chombo hicho cha anga ya juu cha Shenzhou-18 Aprili 25, 2024. Wanaanga hao watatu walirejea duniani Novemba 4 baada ya siku 192 katika obiti, wakiweka rekodi mpya kwa safari moja ya chombo kilichobeba wanaanga iliyokaa kwa muda mrefu zaidi katika anga ya juu kufanywa na wanaanga wa China.
Wakati wa safari hiyo, wanaanga hao wa Shenzhou-18 walitumia rafu za majaribio ya kisayansi na vitu vya kuwezesha mijongeo ya wanaanga ndani na nje ya chombo kufanya majaribio kadhaa katika nyanja za fizikia ya msingi katika mikrograviti, sayansi ya nyenzo katika anga ya juu, sayansi ya maisha katika anga ya juu, matibabu katika anga ya juu na teknolojia ya anga ya juu. Pia walifanya kazi za nje ya chombo kwa mara mbili.
Ye, kamanda wa safari hiyo ya Shenzhou-18, amekuwa mwanaanga wa kwanza wa China aliyekaa zaidi ya mwaka mmoja kwa ujumla katika anga ya juu, akiweka rekodi mpya kwa mwanaganga wa China kukaa muda mrefu zaidi kwenye obiti.
"Nina fahari kushuhudia na kushiriki katika maendeleo makubwa kwenye safari za majukumu ya anga ya juu za China na wanaanga wenzangu," amesema kwenye mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika katika Kituo cha Wanaanga cha China mjini Beijing.
Wanaanga hao wataendelea na mafunzo ya kawaida mara tu watakapofaulu tathmini zote za afya na hali ya mwili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma