Huku Siku 30 zikiwa zimebaki: Harbin yajiandaa kwa kuandaa tena Michezo ya Majira ya Baridi ya Asia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 09, 2025
Huku Siku 30 zikiwa zimebaki: Harbin yajiandaa kwa kuandaa tena Michezo ya Majira ya Baridi ya Asia
Picha iliyopigwa Januari 8, 2025 ikionyesha saa ya kuhesabu siku kuelekea Michezo ya 9 ya Majira ya Baridi ya Asia ya Harbin 2025 mjini Harbin, Mkoa wa Heilongjiang, kaskazini mashariki mwa China. (Xinhua/Xie Jianfei)

HARBIN, China - Wakati inabaki siku 30 kabla ya kufunguliwa kwa Michezo ya 9 ya Majira ya Baridi ya Asia Jumatano wiki hii, mji mwenyeji wa Harbin katika Mkoa wa Heilongjiang, kaskazini mashariki mwa China unaingia katika hatua yake ya mwisho ya maandalizi.

"Sina shaka kwamba Michezo ya 9 ya Majira ya Baridi ya Asia mjini Harbin itakuwa mafanikio mengine makubwa katika historia ya Harakati za Olimpiki barani Asia," amesema Husain Al Musallam, mkurugenzi mkuu wa Baraza la Olimpiki la Asia (OCA).

Ikiwa katika Mkoa wa Heilongjiang kaskazini mashariki mwa China, Harbin itaandaa Michezo hiyo kwa mara ya pili, baada ya hapo awali kuandaa michezo hiyo ya 3 mwaka 1996. Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano iliyotolewa hivi karibuni, mchezo wa mpira wa magongo wa barafu na curling itaanza mapema Februari 3 na 4, mtawalia, huku ratiba ya jumla ikichukua siku 12. Mchezo wa kwanza wa kutolewa medali ya dhahabu utafanyika asubuhi ya Februari 8.

Chini ya kaulimbiu ya "Ndoto ya Majira ya Baridi, Upendo Miongoni mwa Asia," Michezo hiyo hadi sasa imepokea uandikishaji wa wanamichezo 1,275 (wanaume 755 na wanawake 520) kutoka nchi na maeneo 34 kote Asia. Idadi hiyo inatarajiwa kuifanya michezo hiyo kuwa yenye idadi kubwa zaidi ya nchi, maeneo na wanamichezo kushiriki.

Ili kuhakikisha michezo hiyo kufanyika kwa hali ya juu, waandaaji wamekusanya wataalamu wengi wa michezo ya barafu na theluji wenye uzoefu wa ndani na nje ya China. Mashirikisho ya michezo ya kimataifa na ya Asia yameteua wajumbe 12 wa kiufundi na mjumbe msaidizi mmoja wa kiufundi kutoka nchi na maeneo zikiwemo China, Korea Kusini na Japan.

OCA imeteua maafisa wa kiufundi wa kimataifa 151, ambao watafanya kazi pamoja na maafisa 685 wa ndani, wengi wao wakiwa na uzoefu mkubwa kutoka kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing na michezo mingine mikubwa.

Harbin imepanga mashindano 14 ya majaribio tangu Septemba 2024, katika majumba yote ya mashindano na yanahusu aina zote za michezo.

"Shughuli hizo za majaribio zilitathmini uendeshaji wa majumba ya mashindano, vifaa na miundombinu, uungaji mkono wa eneo husika, uongozi na uratibu, vilevile ufanisi katika maeneo mbalimbali ya uendeshaji," amesema Li Guang, mkurugenzi wa Idara ya Mashindano ya Michezo na naibu kamanda wa Kituo cha Kamandi ya Mashindano cha Michezo hiyo.

Katika siku 30 pekee zijazo, Harbin itakaribisha wanamichezo kutoka kote Asia ili kutimiza ndoto zao, huku dunia ikisherehekea michezo ya majira ya baridi na shauku inayowasukuma mbele.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha