Mkutano wa kilele wa AU kuhusu maendeleo ya kilimo wafunguliwa nchini Uganda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 10, 2025
Mkutano wa kilele wa AU kuhusu maendeleo ya kilimo wafunguliwa nchini Uganda
Washiriki wakihudhuria ufunguzi wa mkutano maalum wa kilele wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu kilimo mjini Kampala, Uganda Januari 9, 2025. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

KAMPALA - Mkutano maalum wa kilele wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu kilimo umefunguliwa Alhamisi mjini Kampala, mji mkuu wa Uganda, huku wataalam na maofisa wa serikali wakitafuta hatua za kuimarisha maendeleo ya bara hilo katika sekta ya kilimo.

Mkutano huo wa siku tatu, ambao ulitanguliwa kwanza na mkutano wa mawaziri na utahitimishwa kwa mkutano wa wakuu wa nchi na serikali za Afrika, utapitia Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP), ambao ni mpango wa bara hilo la Afrika wa kuharakisha maendeleo ya kilimo.

Waziri Mkuu wa Uganda Robinah Nabbanja, ambaye alifungua mkutano huo, ametoa wito kwa nchi mbalimbali kushirikiana ili kutekeleza mapendekezo ya sera zilizotolewa. Amesema inasikitisha kwamba bara hilo, ambalo limejaliwa kuwa na ardhi ya kulima na vyanzo vya maji, lakini linaagiza chakula kutoka sehemu nyingine duniani.

"Mkutano huu unapaswa kutoa mapendekezo halisi ya jinsi Afrika inavyoweza kutoka katika hali hiyo. Ili tuhakikishe maisha yetu ya baadaye ya sisi Waafrika, ni lazima tujilishe wenyewe,” Nabbanja amesema.

Frank Tumwebaze, waziri wa Kilimo, Wanyama, na Mambo ya Uvuvi wa Uganda, amesema mkutano huo utatoa mkakati na mpango kazi wa kutekeleza CAADP kwa muongo mmoja ujao.

Mkutano huo unaofanyika chini ya kaulimbiu "Kujenga Mifumo Himilivu ya Kilimo na Chakula," unakuja baada ya mkakati wa kwanza wa CAADP kuzinduliwa mwaka 2003 ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kufikia Ajenda ya Afrika 2063, kwa mujibu wa waziri huyo.

Joseph Sacko, Kamishna wa AU wa Kilimo, Maendeleo Vijijini, Uchumi wa Bluu, na Mazingira Endelevu, amesema mswada wa mkakati mpya ambao utawasilishwa kwa wakuu wa nchi na serikali ili kuipitishwa ni matokeo ya ripoti ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) mwaka 2024 iliyoonyesha kwamba hakuna nchi mwanachama wa AU ambayo ingeweza kufikia malengo ya CAADP ya Malabo ifikapo mwaka huu.

Sacko amesema viongozi hao waliielekeza AUC kuandaa mkakati huo mpya wa miaka 10 utakaoitikia changamoto zinazoikabili Mifumo ya Kilimo na Chakula barani Afrika.

Takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa asilimia zaidi ya 70 ya watu wa bara hilo wanapata mapato ya kuendesha maisha yao kutokana na kilimo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha