AU yapitisha mkakati wa maendeleo ya kilimo kwa muongo ujao

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 13, 2025
AU yapitisha mkakati wa maendeleo ya kilimo kwa muongo ujao
Washiriki wakihudhuria Mkutano Maalum wa Kilele wa Umoja wa Afrika kuhusu Mpango wa Kina wa Maendeleo ya Kilimo wa Afrika (CAADP) mjini Kampala, Uganda Januari 11, 2025. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

KAMPALA - Nchi za Afrika zimepitisha mkakati mpya wa kuendeleza maendeleo ya kilimo na mifumo ya chakula, ambacho ni chanzo cha kujipatia mapato kwa watu wa bara hilo.

Mkakati na mpango kazi wa miaka 10 wa kutekeleza Mpango wa Kina wa Maendeleo ya Kilimo wa Afrika (CAADP), pamoja na nyaraka ya maafikiano yenye kichwa cha Azimio la Kampala, vimetangazwa Jumamosi kwenye hafla ya kuhitimisha Mkutano Maalum wa Kilele wa Umoja wa Afrika kuhusu CAADP mjini Kampala, mji mkuu wa Uganda.

Chini ya mfumo kazi huo mpya, nchi za Afrika zimeazimia kuimarisha uzalishaji endelevu wa chakula kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2035 na kupunguza hasara ya baada ya mavuno kwa asilimia 50.

Pia wamekubaliana kuongeza uwekezaji na ufadhili katika sekta ya kilimo, wakilenga kukusanya dola za Kimarekani bilioni 100 katika uwekezaji wa umma na wa kibinafsi ifikapo Mwaka 2035.

Ili kufikia malengo haya, nchi za Afrika zinahimiza dhamira ya pamoja kutoka kwa serikali, mabunge, wazalishaji chakula, sekta ya kibinafsi na mashirika ya kiraia kubadili maamuzi kuwa matokeo halisi.

"Kwa pamoja, tunaweza kubadilisha mfumo wa kilimo cha mazao ya chakula barani Afrika kuwa mustakabali endelevu na jumuishi," limesema Azimio hilo.

CAADP ilianzishwa mwaka 2003 kwa lengo la kumaliza njaa na kupambana na umaskini. Wakati wa kuanzishwa kwake, nchi za Afrika ziliahidi kutenga asilimia 10 ya bajeti zao za kitaifa katika kilimo, kwa kujikita katika kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo.

Akizungumza mapema katika mkutano huo siku hiyo ya Jumamosi, Rais wa Uganda Yoweri Museveni amehimiza nchi za Afrika kuchukulia kilimo cha kibiashara na uongezaji thamani kama njia ya ustawi wa kiuchumi.

"Kufanya kilimo kiwe cha kibiashara kikamilifu ili kufikia usalama wa chakula na mapato endelevu kwa kushirikiana na makampuni ya kilimo. Kwa familia zenye ardhi ya ekari nne au chini, fuata mkakati wa kilimo cha kina. Kwa familia zilizo na ardhi kubwa, tumia mbinu za kilimo cha eneo pana," Museveni amesema.

Mkutano huo wa siku tatu ulikutanisha pamoja wajumbe zaidi ya 2,000, wakiwemo wataalamu wa kilimo, mawaziri na wakuu wa nchi kutoka zaidi ya nchi wanachama 40 wa AU, kujadili changamoto za bara hilo na mustakabali wa sekta ya kilimo. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha