

Lugha Nyingine
Wachimbaji madini 82 waokolewa, 36 wafariki nchini Afrika Kusini
JOHANNESBURG - Wachimbaji haramu wa madini jumla ya 118 wametolewa chini mgodini na kuletwa juu ya ardhi kwenye operesheni za uokoaji katika mgodi wa dhahabu uliotelekezwa siku ya Jumatatu na Jumanne mjini Stilfontein katika Jimbo la Kaskazini Magharibi nchini Afrika Kusini, huku 36 wamethibitishwa kufariki dunia, kwa mujibu wa polisi.
Huku operesheni za uokoaji zikiingia siku ya pili, "wachimbaji madini haramu jumla ya 118 wamefukuliwa hadi kufikia saa 10:00 jioni (1400 GMT, kwa saa za Afrika Kusini) siku ya Jumanne," amesema msemaji wa Polisi ya Afrika Kusini Athlenda Mathe.
Mathe amesema kuwa siku ya kwanza ya operesheni hizo zilizoanza Jumatatu, ilishuhudia wachimba madini haramu 35 wakiokolewa, watu tisa kati yao wamethibitishwa kufariki. Na katika siku ya pili, "wachimbaji madini haramu jumla ya 83 wamefukuliwa: 56 wakiwa hai na 27 wamefariki."
“Watu wote 82 waliokamatwa wanakabiliwa na mashtaka ya uchimbaji madini kinyume cha sheria, kuingia bila ruhusa na kukiuka Sheria ya Uhamiaji,” amesema.
Pia siku hiyo ya Jumanne, Waziri wa Madini na Rasilimali za Petroli wa Afrika Kusini Gwede Mantashe na Waziri wa Polisi Senzo Mchunu walitembelea mgodi huo kutathmini maendeleo ya operesheni za uokoaji.
Mantashe ameielezea hali ya Stilfontein kuwa ya uhalifu, na kuiita "mashambulizi ya raia wa wageni."
Janga hilo la Stilfontein limekuwa likiendelea kwa miezi kadhaa, huku zaidi ya wachimba madini haramu 1,500 wakitoka chini ya ardhi mgodini hadi sasa. Mwishoni mwa mwaka 2024, miili angalau minane ilitolewa. Wengi wa wachimbaji madini hao haramu wanaaminika kutoka nchi jirani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma