

Lugha Nyingine
Israel na Hamas wafikia makubaliano juu ya kusimamisha mapigano Gaza, viongozi duniani wapongeza
DOHA - Israel na Hamas wamefikia makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa kubadilishana mateka mjini Gaza baada ya juhudi kubwa za upatanishi za Qatar, Misri na Marekani, Waziri Mkuu wa Qatar ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani ametangaza jana Jumatano kwenye mkutano na waandishi wa habari, akisema pande hizo mbili zinazopigana zimefikia makubaliano kuhusu kubadilishana mateka na wafungwa na kurejea kwa utulivu endelevu utakaopelekea usimamishaji vita wa kudumu.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo utaanza Jumapili, Januari 19.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Hamas itaachia huru mateka 33 katika hatua ya kwanza, itakayochukua muda wa wiki sita, kwa mabadilishano na kuachiliwa huru kwa wafungwa wa Palestina.
Mambo halisi ya hatua ya pili na ya tatu yatatangazwa baada ya kukamilika kwa hatua ya kwanza ya makubaliano.
Al Thani amesisitiza Qatar itaendelea kushirikiana na Misri na Marekani, kusimamia utekelezaji wa makubaliano hayo na kushughulikia ukiukaji wowote unaowezekana kutokea.
Amesema, timu za ufuatiliaji kutoka nchi hizo tatu zitahakikisha utekelezaji wa makubaliano hayo na kuchukua hatua hitajika ili kudumisha utulivu.
"Makubaliano haya ni hatua ya kufikia amani endelevu katika eneo hilo, na tunafshirikiana kwa ukaribu na pande zote kuhakikisha mafanikio yake," Al Thani ameeleza.
Rais wa Marekani Joe Biden, akizungumza katika Ikulu ya Marekani, ameyaelezea makubaliano hayo kuwa "moja ya mazungumzo magumu zaidi ambayo nimewahi kuyapitia" na kusisitiza lengo la kumaliza vita hivyo.
Katika muda wa wiki sita zijazo, "Israel itajadiliana kuhusu mipango muhimu ili kuingia hatua ya pili, ambayo ni mwisho wa kudumu wa vita hivyo," Biden amesema.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha makubaliano hayo akisema, "kipaumbele chetu lazima kiwe kupunguza mateso makubwa yanayosababishwa na mgogoro huu."
Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unapenda kuunga mkono utekelezaji wake na kutoa misaada endelevu ya kibinadamu kwa Wapalestina.
Guterres pia ametoa wito kwa pande zote kufanyia kazi "suluhu ya nchi mbili iliyojadiliwa" kama kipaumbele cha dharura.
Hamas imeyasifu makubaliano hayo kuwa ni ushindi, huku afisa mwandamizi wake Khalil al-Hayya akisifu ustahimilivu na moyo wa kujitoa mhanga kwa Wapalestina.
Viongozi wengine waliopokea na kupongeza makubaliano hayo ni, Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abdullah bin Zayed Al Nahyan.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma