

Lugha Nyingine
Watu 246, miili 78 yapatikana kutoka kwenye mgodi haramu nchini Afrika Kusini
JOHANNESBURG - Watu 246 na miili 78 imepatikana na kuletwa juu ya ardhi katika kipindi cha siku tatu za operesheni ya uokoaji kwenye mgodi uliotelekezwa wa dhahabu nchini Afrika Kusini, polisi wamesema katika taarifa yao iliyotolewa Jumatano usiku.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa saa 2 usiku Jumatano, Idara ya Polisi ya Afrika Kusini (SAPS) imesema kuwa wachimbaji haramu wa madini 246 wamepatikana wakiwa hai kutoka chini ya ardhi na wamekamatwa tangu operesheni hiyo ya uokoaji ilipoanza Jumatatu wiki hii kwenye mgodi wa Stilfontein katika Jimbo la Kaskazini Magharibi. Idadi ya miili iliyopatikana imefikia 78, sawa na taarifa iliyotolewa awali siku hiyo saa 10 jioni.
"Hatuwezi kusema kwa uhakika kwamba operesheni imesitishwa kwa hatua hii," msemaji wa kitaifa wa SAPS Athlenda Mathe ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Amesema hayo baada ya watu wa kujitolea waliohusika katika oparesheni hiyo ya uokoaji kuviambia vyombo vya habari kwamba hakukuwa na manusura au miili iliyo chini ya ardhi.
Mathe amesema Idara ya Uokoaji Migodini, ambayo imehusika na operesheni hiyo katika mgodi wa Stilfontein, ilikuwa imepanga kupeleka ngome chini ya ardhi Alhamisi asubuhi "ili kuona kama kuna wachimbaji haramu wowote watavutwa juu na ngome hiyo."
"Tutategemea Idara ya Uokoaji Migodini kuthibitisha hili kwa vifaa vyao vya kisasa. Hiyo tunaweza kujua kile kinachotokea chini ya ardhi," amefafanua. "Tumeonyesha kuwa kama SAPS, tunapaswa kuthibitisha hili."
Msemaji huyo ameongeza kuwa polisi ilikuwa watoe taarifa zaidi kuhusu operesheni hiyo ya uokoaji jana Alhamisi asubuhi.
Hali hiyo katika shimo la migodi isiyotumika huko Stilfontein imekuwa ikiendelea tangu Agosti 2024, wakati vikundi vidogo vya wachimbaji haramu vilipoanza kutoka shimoni. Tangu wakati huo, wachimbaji haramu wapatao 1,576 wametolewa chini ya ardhi na kukamatwa, huku wengi wao wakiwa ni raia wa kigeni kutoka nchi jirani, taarifa za awali za polisi zilieleza.
Migodi mingi ya dhahabu nchini Afrika Kusini ambayo ilifungwa kwa miongo kadhaa kutokana na kupungua kwa uzalishaji imechukuliwa na wachimbaji haramu wa kigeni ambao wanaifungua tena kutafuta dhahabu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma