

Lugha Nyingine
Michezo ya msimu wa baridi yaingiza uhai kwa Mji wa Liupanshui wa China
GUIYANG, China - Katika Eneo la Kuteleza Kwenye Theluji Milimani la Yushe la Liupanshui, Mkoani Guizhou, kusini-magharibi mwa China, watalii waliovalia mavazi ya rangi angavu ya kuteleza kwenye theluji wanapita kwenye miteremko iliyofunikwa na theluji iliyozungukwa na misitu minene.
Likiwa ni eneo la kwanza la mapumziko ya burudani la kuteleza kwenye theluji lenye miinuko ya juu katika mkoa huo wa Guizhou, Eneo la Kuteleza Kwenye Theluji Milimani la Yushe limekuwa likivutia watu wengi wanaopenda mchezo huo tangu lilipoanza kufanya kazi Desemba 2013. Eneo hilo lina njia za kuteleza kwenye theluji kwa wanaoanza kujifunza, wenye uzoefu wa kati na wenye uzoefu wa hali ya juu, likichukua watelezaji kwenye theluji takriban 3,000 kwa wakati mmoja.
Kwenye ukumbi wa eneo hilo, watalii wenyeji na wale kutoka mikoa mingine kama Hainan, Sichuan na Guangdong hukodisha nguo na bodi za kuteleza kwenye theluji.
"Nilishuhudia theluji kwa nadra sana nilipokuwa mtoto, na sikutarajia kujionea na kushiriki mchezo wa kuteleza kwenye theluji milimani katika eneo la mapumziko ya kuteleza kwenye barafu la mazingira ya asili bila kwenda sehemu ya kaskazini ya nchi yetu," amesema Hu Xinyu, mtalii mwenye umri wa miaka 24 kutoka Chongqing.
Katika miaka ya hivi karibuni, mji huo wa Liupanshui umetumia vizuri sifa bora za mazingira yake ya kipekee ya asili ya milima kubadilisha rasilimali zake za theluji kuwa nguvu mpya ya ufungamanishaji wa utamaduni na utalii.
"Kuteleza kwenye theluji si tu mchezo tena. Imekuwa shughuli ya burudani. Tunashuhudia wazi ongezeko la wapenda kuteleza kwenye theluji kila mwaka," amesema Zhang Kai, naibu meneja mkuu wa Kampuni ya Kuendeleza Utalii ya Guizhou Yeyuhai.
Zhang ameongeza kuwa katika msimu wa 2024, Eneo hilo la Yushe limepokea watalii zaidi ya 7,000, huku mauzo ya awali ya mtandaoni yakizidi Yuan milioni 6.5 (dola za Marekani takriban 880,000) na jumla ya mapato kutokana na shughuli husika ikifikia yuan milioni 1.8.
Kwa mujibu wa Chen Tao, mkurugenzi wa Kituo cha Kuendeleza Utalii wa Kitamaduni cha Liupanshui, mji huo umeunda maeneo matatu ya mapumziko ya kuteleza kwenye thelujiyenye miinuko mirefu, hatua kwa hatua ukiunda mfumo wa utalii wa msimu wa baridi na huduma za burudani zinazojikita katika kufungamanisha kuteleza kwenye theluji na chemchemi za maji ya moto.
Maeneo hayo matatu ya kuteleza kwenye theluji yalipokea watalii zaidi ya 200,000 katika msimu wa 2024 wa kuteleza kwenye theluji.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma