Mateka watatu wa Israel wajumuika tena na wanafamilia wao huku usimamishaji vita ukileta hali yenye utulivu ya muda mfupi mjini Gaza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 20, 2025
Mateka watatu wa Israel wajumuika tena na wanafamilia wao huku usimamishaji vita ukileta hali yenye utulivu ya muda mfupi mjini Gaza
Watu wakiwa wamekusanyika uwanjani kukaribisha kurejea kwa mateka watatu wa kwanza wa Israel walioachiliwa kutoka Ukanda wa Gaza baada ya usimamishaji mapigano kuanza kutekelezwa, Tel Aviv, Israel, Januari 19, 2025. (Xinhua/Wang Zhuolun)

JERUSALEM/GAZA - Mateka watatu wa kwanza wa Israel walioachiliwa kutoka Ukanda wa Gaza chini ya makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa rasmi jana Jumapili wamerejea Israel na kujumuika tena na wanafamilia wao. Wakati huo huo, wananchi wa Gaza wamesherehekea kumalizika kwa mashambulizi mabaya ya Israel yaliyodumu kwa zaidi ya miezi 15.

Usimamishaji huo mapigano umemaliza mashambulizi ya Israel ambayo yamegharimu maisha ya Wapalestina zaidi ya 46,900, kwa mujibu wa takwimu za mamlaka ya afya ya Gaza. Mapigano hayo mabaya pia yameharibu sehemu kubwa ya Gaza na kusababisha njaa na magonjwa katika ukanda huo.

Miongoni mwa wanawake hao watatu walioachiliwa huru ni Emily Damari, Mwisrael mwenye asili ya Mwingereza mwenye umri wa miaka 28 na Doron Steinbrecher, mkunga wa mifugo Muisrael mwenye asili ya Mromania mwenye umri wa miaka 30, ambao wote walitekwa nyara kutoka Kibbutz Kfar Aza nje ya kaskazini mwa Gaza, na Romi Gonen, mwenye umri wa miaka 23 ambaye alichukuliwa kutoka kwenye tamasha la muziki la Nova.

Matangazo ya moja kwa moja kutoka Gaza yalionyesha mateka hao, wakiachiliwa huru kutoka mateka ya siku 471, wakihamishwa kutoka kwenye gari la Hamas lililokuwa limezingirwa na wanamgambo wenye silaha hadi kwenye gari la Shirika la Msalaba Mwekundu, ambalo liliwasafirisha hadi kwa vikosi vya Israeli.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imetoa picha za wanawake hao wakikumbatia mama zao kwenye kambi ya kijeshi nje ya Gaza. Baadaye, helikopta ziliwapeleka hadi Kituo cha Matibabu cha Sheba huko Ramat Gan, kitongoji cha Tel Aviv, ambako walipata huduma ya matibabu na kisaikolojia.

Mama yake, Mandy, ameeleza katika taarifa yake ya shukrani kwa waungaji mkono, akisema, "Baada ya siku 471, Emily hatimaye amerudi nyumbani."

Mjini Gaza, shangwe zilizuka mitaani, huku watu wakiimba na kupeperusha bendera ya Palestina. Wakazi waliokimbia makazi yao wameanza kurejea makwao katika maeneo ya kaskazini na kusini, wakija na kukuta miundombinu mingi kubomolewa.

Chini ya makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano, Israel ilikuwa imepanga kuwaachilia huru wafungwa 90 wa Palestina siku hiyo ya Jumapili, hasa wanawake na watoto kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Jerusalem Mashariki. Katika muda wa wiki sita zijazo, Hamas itawaachilia mateka 33 kwa hatua tofauti, wakiwemo wanawake, watoto, wanaume wenye umri wa zaidi ya miaka 50, wagonjwa na waliojeruhiwa.

Miili ya Mateka waliofariki yanatarajiwa kurejeshwa katika hatua za baadaye. Israel inakadiria kuwa karibu nusu ya mateka 98 ambao bado wanashikiliwa huko Gaza wako hai, ingawa Hamas haithibitisha.

Netanyahu ameelezea kuachiliwa huru kwa mateka hao ni "wakati muhimu, wakati wa kusisimua...," akiongeza kuwa mateka hao watatu "walipitia kuzimu."

Wakati huo huo, Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel Daniel Hagari, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, ameonya kuwa jeshi hilo linaongeza nguvu katika Ukingo wa Magharibi na kuendelea kuwa tayari kuchukua hatua za kijeshi kama Hamas itakiuka makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano.

Abu Ubaida, msemaji wa Brigedi za Al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas, amesema Jumapili kwamba Al-Qassam na makundi mengine ya Palestina yana dhamira ya dhati katika makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Renato Lu)

Picha