

Lugha Nyingine
Wanafunzi 52 wa Zimbabwe watunukiwa Ufadhili wa Masomo wa Urafiki kati ya China na Zimbabwe
HARARE - Wanafunzi jumla ya 52 wa lugha ya Kichina nchini Zimbabwe wamepokea ufadhili wa masomo jana Jumanne chini ya mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Urafiki kati ya China na Zimbabwe.
Ikiwa ilizinduliwa mwaka 2020 na Ubalozi wa China nchini Zimbabwe kwa ushirikiano na Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe (CIUZ), mpango huo wa Ufadhili wa Masomo wa Urafiki kati ya China na Zimbabwe unalenga kuunga mkono wanafunzi wa Zimbabwe kumaliza masomo yao.
Wanafunzi wanaopewa ufadhili huo wamechaguliwa kutoka CIUZ, shule za kufundisha lugha ya Kichina zinazoshirikiana na CIUZ, na maeneo mengine ya kufundishia lugha ya Kichina kote Zimbabwe.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa ufadhili wa masomo iliyofanyika kwenye Ubalozi wa China katika mji mkuu wa Harare, Simelisizwe Sibanda, naibu waziri wa elimu ya juu na ufundi, uvumbuzi, sayansi na maendeleo ya teknolojia wa Zimbabwe, ameipongeza China kwa kuunga mkono azma ya Zimbabwe ya kuhakikisha elimu inapatikana kwa wote.
"Programu hii inaendana vyema na itikadi na sera jumuishi ya Zimbabwe ya kutomwacha mtu yeyote na sehemu yeyote nyuma katika ujenzi wa taifa. Kama nchi, msukumo wetu ni kuhakikisha kwamba sisi sote tunashiriki katika ujenzi wa nchi yetu," amesema.
Akizungumza katika hafla ya hiyo, Mkurugenzi wa CIUZ wa Zimbabwe Laston Mukaro amesema mpango huo wa ufadhili wa masomo unaashiria jitihada za China kwa jumuiya yenye ndoto za pamoja, matarajio ya pamoja, na ustawi wa pamoja.
“Kwa kufahamu vyema lugha ya Kichina, wanafunzi si tu wanaboresha ujuzi wao wa mawasiliano lakini pia wanajiweka katika nafasi nzuri ya kufanikiwa katika dunia yenye utandawazi wa uchumi ambapo China ina mchango mkubwa katika biashara, teknolojia na utamaduni,” amesema Mukaro.
Balozi wa China nchini Zimbabwe Zhou Ding amebainisha umuhimu wa kujifunza lugha ya kigeni, akiongeza kuwa katika dunia inayozidi kuunganisha kwa kasi, lugha hutumika kama daraja linalounganisha tamaduni, kuongeza kuelewana, na kuimarisha urafiki.
"Kwa kuifahamu lugha ya Kichina, unafungua hazina ya fursa: kitamaduni, kitaaluma, na ajira. Mnakuwa walinzi wa lugha inayozungumzwa na watu zaidi ya bilioni moja na yenye historia ya maelfu ya miaka," amesema Zhou.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma