Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ahimiza ushirikiano wa kimataifa kushughulikia changamoto zinazoongezeka (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 23, 2025
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ahimiza ushirikiano wa kimataifa kushughulikia changamoto zinazoongezeka
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Uchumi Duniani mjini Davos, Uswizi, Januari 22, 2025. (Xinhua/Lian Yi)

DAVOS, Uswisi – Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa tahadhari kali kuhusu changamoto zinazoongezeka zinazomkabili binadamu, ikiwa ni pamoja na janga la mabadiliko ya tabianchi na mgawanyiko wa siasa za kijiografia, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana kuzishughulikia.

Akihutubia Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Uchumi Duniani mjini Davos, Uswisi, Guterres amesema dunia inakabiliana na "sanduku la matatizo la Pandora" na amesisitiza kuwa ushirikiano ndiyo msingi wa kushughulikia changamoto hizo.

Ameelezea hali mbaya ya dharura ya tabianchi, akilinganisha utegemezi wa binadamu kwa nishati ya mafuta ya kisukuku na "mnyama wa kutisha Frankenstein" ambaye hamwachi salama yeyote.

"Uraibu wetu wa mafuta ya kisukuku ni mnyama wa kutisha Frankenstein, asiye acha salama chochote na yeyote. Kote karibu nasi, tunaona ishara wazi kwamba mnyama huyo amekuwa mtawala," amesema. "Kupanda kwa kiwango cha bahari, mawimbi ya joto, mafuriko, dhoruba, ukame na moto wa nyika ni muhtasari tu wa filamu ya kutisha ya siku za baadaye."

Ametoa wito kwa serikali kutimiza ahadi zao kwa kutoa mipango kazi mipya ya tabianchi kabla ya mkutano wa COP30 wa mabadiliko ya tabianchi nchini Brazil. Pia ametoa wito kwa taasisi za fedha kuunga mkono nchi zinazoendelea kubadilisha muundo wao wa nishati kuwa nishati mbadala.

Guterres ameelekeza msisitizo wake kwenye Akili Mnemba (AI), akikiri uwezo wake wa kuleta mapinduzi katika sekta kama vile afya, elimu, na kukabiliana na janga. Hata hivyo, ameonya dhidi ya hatari zinazoletwa na AI, ikiwa ni pamoja na uwezekano wake wa kuvuruga uchumi na soko la ajira.

Ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na za pamoja ili kukabiliana na changamoto hizo. "Kama jumuiya ya dunia, lazima tuyatekeleza majukumu haya makubwa, na tufanye hivyo kwa kufanya kazi vilevile kwa ushirikiano kama kauli mbiu ya Baraza la Uchumi Duniani."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha