

Lugha Nyingine
Uganda na China zafanya kongamano la kukuza utalii na mawasiliano ya kitamaduni
![]() |
Picha hii iliyopigwa Januari 21, 2025 inaonyesha semina ya Kongamano la Utalii na Utamaduni kati ya Uganda na China ikifanyika mjini Kampala, mji mkuu wa Uganda. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua) |
KAMPALA - Uganda na China zimeandaa Kongamano la siku moja la Utalii na Utamaduni kati ya Uganda na China lenye kaulimbiu ya "Kuunganisha Tamaduni, Kuimarisha Ushirikiano: Kufungua Fursa za Utalii wa Uganda na China," mjini Kampala, mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika, ili kuhimiza maendeleo ya utalii na mawasiliano ya utamaduni kati ya pande hizo mbili.
Kongamano hilo la kwanza, ambalo limefanyika siku ya Jumanne limeleta pamoja maafisa wa serikali, wadau wa sekta ya utalii, na waendeshaji biashara ya utalii kutoka Uganda, China, na ukanda wa Afrika Mashariki.
Akiangazia fursa kubwa kwa Uganda na China kushirikiana katika kukuza utalii, Waziri wa Utalii, Wanyamapori na Mambo ya Kale wa Uganda Tom Butie amesema pande zote mbili zinaweza kutumia kikamilifu fursa za vitu vya urithi wa kitamaduni na vivutio vya watalii vya kupendeza ili kuendeleza maendeleo ya nchi hizo mbili.
Amesema, Uganda ina shauku ya kufaidika kikamilifu katika soko linaloshamiri la watalii wanaosafiri nje la China, ikipata hamasa kutoka kwa mikakati ya China yenye mafanikio ya utalii wa ndani huku ikitafuta fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.
"Uganda inazingatia sana soko la China, ambalo linawakilisha fursa muhimu ya kukuza sekta yetu ya utalii. Urithi tajiri wa kitamaduni wa China na utalii wa kusafiri nje unaokua kwa kasi unaifanya kuwa mwenzi wetu tunapojitahidi kuendeleza huduma mpya za utalii," amesema waziri huyo.
Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong amesema kongamano hilo linawakilisha hatua muhimu katika ushirikiano kati ya Uganda na China katika sekta ya utalii, likiingiza nguvu mpya katika urafiki kati ya China na Uganda.
Amesema nchini China, utalii unatoa mchango mkubwa katika kupunguza umaskini, kutengeneza fursa za ajira na kuongeza mapato ya fedha za kigeni, ambapo vyote vinahimiza ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii.
Dai Bin, Mkuu wa taasisi ya utafiti wa Utalii ya China, amewasilisha makala kuhusu kuweka mfano wa Uganda wa ushirikiano wa utalii kati ya China na Afrika, akibainisha kuwa kutokana na kuimarika kwa kasi kwa utalii wa dunia, mawasiliano na ushirikiano wa utalii kati ya China na Uganda unaingia katika kipindi kipya cha fursa ya kimkakati.
Utalii ni sekta inayoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni nchini Uganda, ikileta dola za Kimarekani zaidi ya bilioni kwa mwaka, kwa mujibu wa wizara hiyo ya Uganda.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma