

Lugha Nyingine
Watoto wa Tanzania wafanyiwa upasuaji wa moyo kwa kutumia teknolojia mpya iliyoongozwa na China (4)
![]() |
Husna Shabaan Kingwande, mama wa Ikram, akizungumza na Shirika la Habari la China, Xinhua baada ya upasuaji wa moyo wenye mafanikio wa mtoto wake katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam, Tanzania, Januari 18, 2025. (Xinhua) /Emmanuel Herman) |
DAR ES SALAAM - Machozi ya furaha yalikuwa yakitiririka wakati Husna Shabaan Kingwande alipoambiwa kuwa upasuaji wa moyo wa mtoto wake Ikram mwenye umri wa miaka mitatu umekuwa wenye mafanikio ambapo upasuaji huo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyojengwa na China jijini Dar es Salaam, Tanzania, umeashiria hatua kubwa ya kuanzishwa kwa teknolojia ya hali ya juu ya tiba ya China nchini Tanzania.
Ikram alikuwa ni miongoni mwa watoto watano, wenye umri wa kati ya miaka mitatu na saba, ambao wamefanyiwa upasuaji huo wa moyo na mishipa kwa kutumia Utaratibu wa PAN, mbinu ya upasuaji wenye majeraha madogo iliyoanzishwa na Profesa Pan Xiangbin wa Hospitali ya Fuwai ya China.
Utaratibu huu wa kimapinduzi, ambao hutegemea picha ya ultrasound badala ya njia ya kawaida ya fluoroscopy, hutibu magonjwa ya moyo na mishipa kupitia mishipa ya damu bila kufanyiwa upasuaji wa kufungua moyo au kuchomwa mionzi.
Upasuaji huo umefanywa na timu ya wataalam tiba watano kutoka China, wataalamu sita wa Tanzania kutoka JKCI, na mtaalam mmoja wa kundi la 27 la timu ya madaktari wa China waliopo katika taasisi hiyo.
Kwa Kingwande, mzaliwa wa Mkoa wa Pwani wa Tanzania mwenye umri wa miaka 22, upasuaji wa mtoto wake wa kiume wenye mafanikio unamaanisha mustakabali mwema kwa mtoto huyo ambaye alithibitishwa kuwa na ugonjwa wa moyo na kuanza kutibiwa miezi tisa iliyopita.
“Nawashukuru sana madaktari wa China na wenzao wa Tanzania kwa kumpa maisha mapya mwanangu,” amesema huku machozi yakitiririka.
Shukurani pia zimetolewa na Ajili Anthony Msunza, baba wa watoto wawili kutoka mkoani Mbeya, Kusini Magharibi mwa Tanzania ambaye mtoto wake Noreen mwenye umri wa miaka mitano alikuwa miongoni mwa wagonjwa hao watoto.
"Teknolojia hii mpya imefufua matumaini kwa wagonjwa wa moyo nchini Tanzania," amesema.
Utaratibu wa PAN unawakilisha maendeleo makubwa katika matibabu ya moyo.
Wakati wa kipindi cha mafunzo katika JKCI, Pan alieleza kuwa mbinu hiyo inawezesha wagonjwa kuendelea kuwa na ufahamu wakati wa matibabu, kuondoa hitaji la maabara za matibabu ya tiba za moyo yanayotumia mionzi.
"Utaratibu huu si tu ni salama na wenye ufanisi zaidi lakini pia hufanya matibabu ya moyo kupatikana katika kliniki," amesema.
Theophylly Ludovick, ni daktari wa watoto wa JKCI ambaye hivi karibuni alipatiwa mafunzo ya mbinu za utaratibu wa PAN nchini China.
Ludovick anasisitiza uwezekano mkubwa wa utaratibu huo katika kukabiliana na mzigo mkubwa wa Tanzania wa magonjwa ya moyo na mishipa, ambapo mtoto mmoja kati ya 100 ana matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo.
"Ushirikiano huu kati ya China na Tanzania ni hatua muhimu katika kuokoa maisha na kuimarisha uhusiano wa pande mbili," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma