

Lugha Nyingine
Vitoto vya Panda vyatuma salamu za Mwaka Mpya wa Jadi wa China kutoka kusini magharibi mwa China
CHENGDU – Vitoto 25 vya panda vimekusanywa katika vituo viwili vya kuzaliana kwa panda katika Mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China siku ya Alhamisi kutuma salamu za Mwaka Mpya wa Jadi wa China kwa watazamaji wa kimataifa ambapo vitoto hivyo vyote vya panda vilizaliwa mwaka jana 2024 -- 13 katika Kituo cha Uhifadhi na Utafiti wa Panda cha China, na 12 katika Kituo cha Utafiti wa Kuzaliana kwa Panda cha Chengdu.
Katika eneo kikuu la panda la Shenshuping la Kituo cha Uhifadhi na Utafiti wa Panda cha China, vitoto hivyo 13 vilizunguka katika eneo hilo, ambalo lilikuwa limepambwa kwa vyakula vya kijadi vya China kama vile Tanghulu (matunda ya peremende) na mapambo yakiwemo ya midoli yenye umbo la nyoka kusherehekea Mwaka mpya ujao wa Nyoka wa China.
Wakati huo huo, vitoto vingine 12 vya panda vilionekana kwenye kituo cha Chengdu, ambacho kilikuwa kimepambwa kwa taa za kijadi na vitu vingine vilivyo na mambo ya urithi wa utamaduni usioshikika, kama vile karatasi za kukatwa kisanii.
Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China mwaka huu, kwa kalenda ya kilimo ya China, itaangukia Januari 29.
Mashirika hayo mawili yanaunda kituo kikuu cha kitaifa cha uhifadhi na utafiti wa panda, jukwaa la hadhi ya kimataifa lililozinduliwa mwaka 2023 kwa ushirikiano wa utafiti na mabadilishano ya panda.
Kwa miaka mingi, mashirika hayo yamekuwa yakishirikiana katika ulinzi wa panda na mabadilishano ya kitaaluma, yakipata mafanikio katika maeneo makuu ya utafiti kama vile ulinzi wa idadi na makazi ya panda.
Mashirika hayo mawili pia yamekusanya majopo ya wataalam kuunga mkono Hifadhi ya Kitaifa ya Panda, ambayo ilianzishwa mwaka 2021 na ikienea kwa ukubwa katika sehemu za mikoa ya Sichuan, Shaanxi na Gansu.
Shukrani kwa juhudi za ulinzi, Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira ya Asilia ulishusha hadhi ya panda kutoka wanyama walio hatarini kutoweka hadi walio katika hali hatarishi.
Takwimu rasmi zinaonyesha idadi ya panda wa mwituni nchini China imeongezeka kutoka karibu 1,100 katika miaka ya 1980 hadi karibu 1,900. Idadi ya panda wa kufugwa katika maeneo maalum duniani sasa inafikia 757.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma