Kituo cha Vyombo vya Habari cha Michezo ya Majira ya Baridi ya Asia ya Harbin chaanza kufanya kazi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 01, 2025
Kituo cha Vyombo vya Habari cha Michezo ya Majira ya Baridi ya Asia ya Harbin chaanza kufanya kazi
Picha iliyopigwa Januari 31, 2025 ikionyesha kituo kikuu cha vyombo vya habari cha Michezo ya Majira ya Baridi ya Asia Mwaka 2025 mjini Harbin, Mkoa wa Heilongjiang, kaskazini mashariki mwa China. (Xinhua/Zhag Tao)

HARBIN – Ikiwa imebaki wiki moja kabla ya hafla ya ufunguzi wa Michezo ya Majira ya Baridi ya Asia Mwaka 2025 mjini Harbin, Mkoa wa Heilongjiang, kaskazini mashariki mwa China, Kituo Kikuu cha Vyombo vya Habari (MMC) cha michezo hiyo kimeanza kufanya kazi rasmi jana Ijumaa.

Kikiwa kinapatikana katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano, Maonyesho na Michezo cha Harbin, kituo hicho kina Kituo Kikuu cha Waandishi wa Habari (MPC) na Kituo cha Kimataifa cha Utangazaji (IBC).

Watu wa kujitolea katika kituo hicho wamekuwa tayari kutoa huduma za lugha na uelekezaji kwa waandishi na watangazaji wa habari wa vyombo vilivyosajiliwa, na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni katika kituo hicho pia yanapatikana. Katika duka la bidhaa rasmi za Michezo ya tisa ya Majira ya Baridi ya Asia, aina mbalimbali za vitu vya ukumbusho ikiwa ni pamoja na maskoti simbamarara wa kupendeza "Binbin" na "Nini" wa michezo hiyo vimevutia macho ya wengi.

"MMC kitafanya kazi kwa saa 24 kikiwa na huduma kamili za IPTV, au TV za Protokali ya Intaneti, wakati wa Michezo hiyo," ameeleza Lyu Zhuangzhi, mkurugenzi wa uendeshaji wa vyombo vya habari wa MMC.

MPC kinajumuisha chumba cha mkutano na waandishi wa habari, kituo cha habari cha mtandaoni, na vyumba vya kazi vya vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na Shirika la Habari la China, Xinhua, ambalo ni shirika la habari mdhamini wa michezo hiyo. Aidha, MPC pia kinaonyesha mienge ya michezo iliyotangulia ya Michezo ya Majira ya Baridi ya Asia na kinaonyesha kazi za maandishi ya Kaligrafia ya Kichina na picha za kuchorwa zenye maudhui ya Michezo ya Harbin 2025.

Pia siku hiyo ya Ijumaa, Kijiji cha Wanamichezo kando ya MMC na Kituo cha Habari cha Mlimani kwa michezo ya theluji katika eneo la Yabuli kilianza kufanya kazi rasmi.

Mechi ya kwanza ya michezo hiyo ya majira ya baridi ya Asia ya Harbin itaanza Jumatatu kwa mchezo wa mpira wa magongo wa barafu kabla ya hafla ya ufunguzi Februari 7. Michezo hiyo itamalizika Februari 14. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha