

Lugha Nyingine
Ushirikiano wa uvuvi kati ya China na Guinea Bissau wastawi huku meli za uvuvi zikianza safari za kwanza za msimu huu (4)
![]() |
Picha iliyopigwa Februari 2, 2025 ikionyesha soko la samaki kwenye Bandari ya Uvuvi ya Bandim mjini Bissau, mji mkuu wa Guinea-Bissau. (Xinhua/Si Yuan) |
BISSAU - Katika pwani ya Bahari ya Atlantiki ya Guinea-Bissau, mwanga wa jua ulikuwa uking'aa kwenye bahari inayotiririka. Kwenye Bandari ya Uvuvi ya Bandim, wafanyakazi wa Kampuni ya Uvuvi ya China (CNFC) nchini Guinea-Bissau walikuwa wakirekebisha nyavu za uvuvi na kukagua hali ya uwepo wa mafuta, wakifanya maandalizi ya mwisho kwa safari za kwanza za mwaka huu za uvuvi.
Huku miluzi mikali ikipenya hewani, meli saba za uvuvi ziliondoka kutoka kwenye bandari, zikielekea bahari yenye kina kirefu. Vipuli vyao vilikuwa viking'aa chini ya mwanga wa jua uliokuwa ukififia wakati meli hizo zikitawanyika kwenye mawimbi, na kuacha nyuma vijia vya povu jeupe.
Qi Lianghua, nahodha mwenye umri wa miaka 54 wa meli ya uvuvi ya Yuanyu 884, amekuwa akivua samaki katika maji ya Guinea-Bissau kwa miaka 28 mfululizo. Amesema, safari hii inajumuisha wafanyakazi 101 wa China na wafanyakazi 127 wa kigeni. Huku Guinea-Bissau ikitekeleza kusimamishwa kwa shughuli za uvuvi kila Januari, meli hizo huanza safari Februari 1 kila mwaka, zikitumia hadi miezi 11 baharini.
"Wafanyakazi wetu hula samaki kila mlo, hivyo kila meli ya usambazaji inapoleta mboga freshi za majani, watu wote wanafurahi," amesema.
Guinea-Bissau ni moja ya nchi zenye rasilimali nyingi za uvuvi katika Bahari ya Atlantiki. Ikiwa na rafu ya bara inayoenea urefu wa kilomita 160 na eneo la kipekee la kiuchumi baharini linalofunika takriban kilomita za mraba 70,000, maji yake yamejaa samaki wa magamba, kamba, kambakoche, kaa na sefalopodi.
Uzalishaji wa samaki kwa mwaka unafikia kati ya tani 300,000 na 350,000. Hata hivyo, kutokana na nchi hiyo kukosa meli zake za uvuvi katika bahari kuu, kutoa leseni za uvuvi kwa meli za kigeni imekuwa moja ya vyanzo vyake vya fedha za kigeni.
Mwezi Agosti 1984, serikali za China na Guinea-Bissau zilitia saini makubaliano ya ushirikiano wa uvuvi kabla ya CNFC kupeleka meli zake za kwanza za uvuvi wa maji ya mbali nchini humo mwezi Mei 1985.
"Hapo zamani, meli zetu zilibeba mamia ya tani za vifaa vya ujenzi wa meli na vifaa vya uvuvi na zilitumia siku 62 kuvuka bahari," amekumbushia Wang Songjie, nahodha wa meli ya uvuvi ya Yuanyu 883 mwenye umri wa miaka 57. "Wakati huo, Bandari ya Bissau haikuwa na vifaa muhimu vya kupakua na vyombo vya usafirishaji. Kila kitu kilipaswa kufanywa kwa mikono."
Mwezi Mei 2023, Bandari ya Uvuvi ya Bandim iliyojengwa kwa msaada wa China ilizinduliwa. Mwaka huo huo, CNFC ilikamilisha kiwanda cha usindikaji na uhifadhi ya samaki karibu na bandari, chenye ukubwa wa takriban mita za mraba 4,000. Sasa kikiwa ni kiwanda kikubwa zaidi cha kisasa cha usindikaji wa mazao ya uvuvi nchini Guinea-Bissau, kinawapa wakazi wenyeji samaki kwa bei nafuu kila wakati.
Issumaila Djalo, mfanyakazi katika ofisi ya CNFC ya Guinea-Bissau, amesisitiza uvuvi kama "moja ya sekta muhimu za Guinea-Bissau". "Shukrani kwa uungaji mkono wa China, rasilimali za baharini za nchi yetu zinanufaisha watu kweli."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma