Rais Cyril Ramaphosa asema Afrika Kusini kuzidisha mageuzi ili kuendesha ukuaji jumuishi (5)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 07, 2025
Rais Cyril Ramaphosa asema Afrika Kusini kuzidisha mageuzi ili kuendesha ukuaji jumuishi
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akitoa Hotuba kwa Taifa kwenye Ukumbi wa Jiji la Cape Town mjini Cape Town, Afrika Kusini, Februari 6, 2025. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)

CAPE TOWN - Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini Alhamisi jioni wakati akitoa Hotuba ya kwa Taifa (SONA), chini ya kaulimbiu "Taifa linalofanya kazi kwa wote," kwenye Ukumbi wa Jiji la Cape Town kabla ya kikao cha pamoja cha mabaraza mawili ya bunge la nchi hiyo amesema kuwa serikali yake itaanzisha wimbi jipya la mageuzi ili kuhimiza ukuaji jumuishi wa uchumi ambao unanufaisha raia wote.

Hii ni hotuba ya kwanza kwa taifa chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) iliyoundwa baada ya uchaguzi wa mwaka 2024 nchini humo.

Kwenye hotuba hiyo, rais ameorodhesha kazi ya serikali katika kutekeleza vipaumbele vitatu vya kimkakati vya Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati: kuhimiza ukuaji jumuishi wa uchumi na kuongeza ajira, kupunguza umaskini na kukabiliana na gharama za juu za maisha, na kujenga nchi yenye uwezo, maadili na maendeleo.

Kwa mujibu wake, Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati ulipitishwa hivi karibuni na GNU, ambao umeweka mpango ulio wazi na kabambe kwa miaka mitano ijayo.

“Kazi yetu ya haraka zaidi ni kukuza uchumi wetu ili tuweze kuongeza ajira, kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya Waafrika Kusini wote,” amesema Ramaphosa, akiongeza kuwa "Tunataka taifa lenye uchumi unaostawi ambao unanufaisha wote. Ili kujenga mzunguko huu mzuri wa uwekezaji, ukuaji na ajira, ni lazima kuongeza ukuaji wa uchumi hadi zaidi ya asilimia 3."

"Katika mwaka ujao, tutaanzisha wimbi la pili la mageuzi ili kuanzisha ukuaji zaidi wa haraka na jumuishi," Ramaphosa amebainisha.

Kwa upande wa masuala ya kimataifa, Rais Ramaphosa amedokeza kwamba Afrika Kusini ilichagua "Mshikamano, Usawa, na Uendelevu" kuwa kaulimbiu ya urais wake wa Kundi la nchi 20 (G20), ambao nchi hiyo iliuchukua Desemba 1, 2024, ili kusisitiza haja ya ushirikiano na uhusiano wa kiwenzi kati ya nchi mbalimbali duniani.

"Kwa mara ya kwanza katika historia, Mkutano wa G20 unaandaliwa katika Bara la Afrika kufuatia Umoja wa Afrika kuwa mwanachama wa G20. Ni fursa ya kuweka mahitaji ya Afrika na pande nyingine za Nchi za Kusini kwa uthabiti zaidi kwenye ajenda ya maendeleo ya kimataifa," amesema.

Huku Afrika ikiendelea kuwa katikati ya sera ya kigeni ya nchi hiyo, "urais wetu wa G20 ni fursa adhimu kwa Afrika Kusini kusongesha mbele juhudi kuelekea ukuaji mkubwa wa uchumi wa dunia na maendeleo endelevu," ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha