

Lugha Nyingine
Goma ya DRC inayokaliwa kimabavu yaripotiwa kuwa katika janga, wafanyakazi wa kibinadamu wahofia milipuko ya magonjwa (3)
![]() |
Wafanyakazi wa afya wakihamisha miili ya watu waliouawa katika mapigano mjini Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Februari 5, 2025. (Picha na Zanem Nety Zaidi/Xinhua) |
UMOJA WA MATAIFA - Vivian van de Perre, naibu mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Goma inayokaliwa kimabavu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amesema siku ya Jumatano kuwa mji huo uko katika janga huku wafanyakazi wa kibinadamu wakipambana na hatari za magonjwa ya mlipuko wakati huohuo wakitoa misaada.
"Mjini Goma, tunaendelea kuwa chini ya uvamizi; hali bado ni tete sana, huku kukiwa na hatari inayoendelea ya kuongezeka kwa mgogoro," amesema kwenye mkutano wa njia ya video na waandishi wa habari.
Amesema waasi wa M23 na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) wanaendelea kuimarisha udhibiti wao juu ya Goma na maeneo mengi ya Jimbo la Kivu Kaskazini ambayo kundi hilo lenye silaha liliyateka hapo awali.
"Njia zote za kutoka Goma ziko chini ya udhibiti wao, na uwanja wa ndege, pia chini ya udhibiti wa M23, umefungwa," van de Perre amesema akiongeza kuwa "Ghasia zinazoongezeka zimesababisha mateso makubwa ya binadamu, kukimbia makazi na kuongezeka kwa janga la kibinadamu."
Van de Perre amesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, unaojulikana kama MONUSCO, pia unafanya kazi katika mazingira yenye changamoto nyingi kwani maeneo yake muhimu katika kituo cha kikanda yamezidiwa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na Wakongo wanaotafuta hifadhi.
"Sehemu hizi za Umoja wa Mataifa hazikuundwa wala kupangwa kwa ajili ya watu wengi kwa muda mrefu" ameongeza huku akisema shinikizo kwenye rasilimali muhimu -- kama vile maji, chakula, usafi wa mazingira na makazi -- linaongezeka.
"Pamoja na vizuizi hivi, MONUSCO inaendelea kulinda wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na kuwapa hifadhi watu walio katika mazingira hatarishi chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu," van de Perre amesema, akisisitiza kwamba "wafanyakazi wa kimataifa na wale wenyeji wa Umoja wa Mataifa wasio na umuhimu wamehamishwa, huku MONUSCO na wafanyakazi wa kibinadamu muhimu wakiendelea kutoa ulinzi na msaada."
Amesema tathmini mpya kutoka timu ya Umoja wa Mataifa nchini humo ni kwamba miili takriban 2,000 imeopolewa kutoka mitaani, huku miili mingine 900 ikiwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti. Pia, bado kuna miili mingi inanayoendelea kuharibika ambayo haijakusanywa. Pia amesema, mbali na wasiwasi kuhusu milipuko ya magonjwa, maafisa wana wasiwasi kuhusu kuzuka kwa ghasia za kikabila.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma