

Lugha Nyingine
"Supamaketi ya Dunia" yafunguliwa tena baada ya likizo, ikikumbatia uvumbuzi katika Mwaka wa Nyoka
HANGZHOU - Soko la Biashara ya Kimataifa la Yiwu, soko kubwa zaidi duniani la mauzo ya bidhaa ndogo ndogo lililo katika Mji wa Yiwu Mkoani Zhejiang, mashariki mwa China, limefunguliwa tena jana siku ya Jumapili baada ya likizo ya Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi, ikiashiria mwanzo mzuri wa Mwaka wa Nyoka, kwa kalenda ya kilimo ya China.
Hafla ya kufunguliwa tena kwa soko hilo ilipambwa na ngoma za jadi za simba na maonyesho ya kupiga ngoma, ikileta hali ya shangwe na shamrashamra.
Wafanyabiashara kama mmiliki wa duka la midoli Chen Meijun wameeleza matumaini kwa mwaka huu wenye mafanikio ulio mbele.
"Tulipokea maulizo kutoka kwa wateja wakati wa likizo, na tunatarajia mauzo kukua kwa zaidi ya asilimia 10 mwaka huu," Chen amesema, akibainisha kuwa anapanga kupanua biashara yake kimataifa, huku safari za kwenda Mexico na Kenya zikiwa zimepangwa mwaka huu.
Ikiwa inafahamika pia kwa jina la "Supamaketi ya Dunia," Yiwu ni kituo cha kimataifa cha uzalishaji wa bidhaa ndogo na biashara, ikivutia wateja kutoka kote duniani.
Mteja kutoka Nepal Raj Kumar Khadka ni miongoni mwa wateja wa kwanza kuwasili, akipanga kuagiza kauri, vyombo vya kioo na bidhaa nyingine zenye thamani ya Yuan karibu milioni 1 (dola za Kimarekani kama 139,500)
Akiwa anakuja mara kwa mara katika soko hilo ambaye alikuja kwa mara ya kwanza kufanya biashara miaka 23 iliyopita, Khadka amesema Yiwu ina mchango muhimu katika biashara ya kimataifa ya bidhaa.
"Yiwu ilinifundisha namna ya kufanya biashara," amesema. "Kwa sababu ya mji huu, niliweza kukutana na watu kutoka duniani kote na kujifunza kuhusu lugha na tamaduni zao."
Maduka 75,000 katika soko hilo yameunganishwa na kampuni za biashara zaidi ya milioni 2.1, zikitoa nafasi za ajira takriban milioni 32. Mahitaji yake makubwa ya ununuzi na ofa mbalimbali za bidhaa zinaonesha uhimilivu na uwezekano wa ukuaji wa uchumi wa China.
Kampuni nyingi za biashara katika soko hilo zinatumia mitindo ibuka, kama vile midoli iliyochapishwa ya 3D, ambayo imepata umaarufu kwa rangi zake maridadi na miundo mizuri.
Mwishoni mwa mwaka 2024, Baraza la Serikali la China liliidhinisha mpango wa jumla wa kuzidisha mageuzi ya kina ya biashara ya kimataifa katika mji huo wa Yiwu, ambao unaelezea maono ya kuhimiza mageuzi kupitia kufungua mlango zaidi, pamoja na mipango kama vile ubunifu wa mifumo ya biashara ya ununuzi wa soko, kuhimiza maendeleo ya biashara ya kuagiza bidhaa nje, kuimarisha kazi za jumla za maeneo ya bandari maalum, na kuimarisha kanuni za biashara ya kuvuka mipaka.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma