Scholz akosoa mpango wa Trump wa Gaza akiuita "kashfa" kwenye mdahalo wa televisheni

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 10, 2025
Scholz akosoa mpango wa Trump wa Gaza akiuita
Picha hii skrini kutoka kwenye matangazo ya moja kwa moja mtandaoni ya shirika la kimataifa la utangazaji linalomilikiwa na serikali ya Ujerumani Deutsche Welle (DW) Februari 9, 2025, ikionyesha Chansela Olaf Scholz wa Ujerumani akiwa kwenye mdahalo wake wa kwanza wa televisheni na Friedrich Merz, kiongozi wa chama cha upinzani cha Christian Democratic Union (CDU), kabla ya uchaguzi wa Bunge la Ujerumani, Bundestag, Februari 23.

BERLIN - Chansela wa Ujerumani Olaf Scholz jana Jumapili jioni kwenye mdahalo wa kwanza wa televisheni na mpinzani wake Friedrich Merz, kiongozi wa chama cha upinzani cha Christian Democratic Union (CDU) kabla ya uchaguzi wa Bunge la Ujerumani, Bundestag utakaofanyika Februari 23, amekosoa mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani kuhamisha Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza, akiuita “ni kashfa."

Moja ya mada kuu zilizojadiliwa ni namna Ujerumani inavyopaswa kushirikiana na Marekani chini ya utawala wa Trump. Akizungumzia suala la Mashariki ya Kati, Scholz amesisitiza upingaji wake kwa pendekezo hilo la Trump kuhusu Gaza.

Awali akizungumza kwenye tukio la kampeni siku ya Ijumaa, Scholz ameeleza kutoridhia kwake, akisema, "Hatupaswi kuwahamisha makazi watu wa Gaza hadi Misri," na kueleza kukataa kabisa mpango huo.

Kwenye mdahalo huo wa jana Jumapili, Scholz ameelezea mkakati wake wa kukabiliana na Trump kuwa unahusisha "maneno ya wazi na mazungumzo ya kirafiki."

Kwa upande wake Merz, ingawa pia ameelezea wasiwasi wake juu ya pendekezo hilo la Trump, amelielezea kama "sehemu ya mapendekezo kadhaa ya kukera kutoka Utawala wa Marekani."

Hata hivyo, amependekeza kwamba Ujerumani inapaswa kusubiri kuona ni mipango gani ambayo serikali ya Marekani inakusudia kutekeleza "kwa umakini."

Kuhusu suala la uwezekano wa Marekani kutoza ushuru, Scholz amethibitisha kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari "kuchukua hatua ndani ya saa moja" kama itahitajika.

Merz, wakati huo huo, amesisitiza umuhimu wa umoja wa Ulaya, ikiwemo ushirikiano na Uingereza licha ya Brexit, akitoa wito wa "mkakati wa pamoja wa Ulaya" ili kukabiliana na changamoto.

Mdahalo wao pia ulihusu masuala muhimu ya ndani, ikiwa ni pamoja na uchumi, uhamiaji, na athari ya mgogoro unaoendelea nchini Ukraine.

Chaguzi zijazo za mapema zinaonekana kama mtihani muhimu kwa Chama cha Scholz cha Social Democratic (SPD), ambacho kwa sasa kina asilimia 16 kwenye kura za maoni. Chama cha kihafidhina cha CDU na chama dada chake cha Bavaria, Christian Social Union (CSU), vinaongoza katika kura za maoni kwa uungwaji mkono thabiti wa asilimia karibu 30.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha