Viongozi wa Afrika watoa wito wa kusimamishwa mara moja mapigano mashariki mwa DRC (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 10, 2025
Viongozi wa Afrika watoa wito wa kusimamishwa mara moja mapigano mashariki mwa DRC
Rais William Ruto wa Kenya akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) jijini Dar es Salaam, Tanzania, Februari 8, 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)

DAR ES SALAAM - Viongozi wa Afrika wametoa wito wa "kusimamishwa mara moja kwa mapigano" mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kusisitiza tena uungaji mkono wao kamili wa kutafuta suluhu ya kudumu kwa mgogoro huo unaoendelea.

"Mkutano wa kilele wa kihistoria," ulioandaliwa kwa pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), jumuiya mbili kuu za kikanda, umefanyika Jumamosi katika Mji wa Dar es Salaam nchini Tanzania kushughulikia mgogoro huo unaoendelea mashariki mwa DRC.

Katika taarifa ya mwisho, viongozi hao wa kikanda wametoa wito wa "kusimamishwa mapigano mara moja" na kurejeshwa kwa njia za usambazaji wa huduma nchini DRC, kwani Kundi la M23 limeripotiwa kusonga mbele kuelekea Bukavu, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kusini, baada ya kuanzisha kile kinachoitwa utawala wake mjini Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini na kituo kikuu cha kikanda.

Kwa kutambua udharura wa hali hiyo, viongozi waliohudhuria mkutano huo wameagiza Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi ya EAC-SADC kukutana ndani ya siku tano ili kupanga mbinu za kitaalamu za kutekeleza usimamishaji huo wa mapigano mara moja na bila masharti.

Viongozi hao wamehimiza kufunguliwa tena kwa njia za barabara ili kurejesha njia za usambazaji wa misaada ya kibinadamu, haswa barabara inayounganisha Goma na Bukavu, ambayo imezuiliwa na waasi wa M23, na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Goma, ambao uliharibiwa vibaya wakati wa mapigano.

Mazungumzo ya kisiasa na kidiplomasia ndiyo suluhu endelevu zaidi kwa mgogoro huo wa mashariki mwa DRC, taarifa hiyo imesema, huku viongozi hao wa kikanda wakionyesha kuunga mkono kurejesha mazungumzo ya moja kwa moja na pande zote za serikali na zisizo za kiserikali, ikiwa ni pamoja na M23, chini ya mifumo iliyopo ya upatanishi wa kikanda.

DRC imekataa aina yoyote ya mazungumzo ya moja kwa moja na M23 lakini imedokeza kufufua Mchakato wa Amani wa Nairobi, mpango wa amani unaoongozwa na EAC na kuwezeshwa na Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Katika taarifa hiyo, nchi hizo za kikanda zimependekeza kuunganisha Mchakato wa Nairobi na Mchakato wa Luanda, utaratibu sambamba wa amani ulioanzishwa na Umoja wa Afrika na kusimamiwa na Rais wa Angola Joao Lourenco.

Michakato yote hiyo miwili ya amani imekabiliwa na vikwazo. Mchakato wa Nairobi umefikia "kugonga mwamba," kwa mujibu wa msemaji wa Kenyatta, Kanze Dena, ambaye alitoa kauli hiyo siku ya Alhamisi, wakati mkutano wa kilele wa amani chini ya Mchakato wa Luanda ulifutwa ghafla dakika za mwisho mwishoni mwa Desemba mwaka jana.

Ili kuunga mkono "Mchakato wa Luanda na Nairobi" uliounganishwa, viongozi hao wa kikanda wamependekeza kuteua wawezeshaji zaidi, ikiwa ni pamoja na wawakilishi kutoka kanda nyingine za Afrika, taarifa hiyo imeeleza.

Mkutano huo umeitishwa ili kuzuia mgogoro huo kuongezeka na kuwa vita vya kikanda. "Kama itaendelea hivi, vita vinaleta hatari ya kuenea katika kanda," Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alionya mapema Februari.

Mgogoro kati ya M23 na serikali ya DRC unahusishwa sana na matokeo ya mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994 na mivutano ya kikabila inayoendelea, haswa kati ya Watutsi na Wahutu.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesisitiza dhamira ya Tanzania ya kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na EAC, SADC na jumuiya ya kimataifa kutatua mgogoro huo wa DRC.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha