

Lugha Nyingine
Bunge la Afrika Kusini laanza kutumia kuba kama ukumbi wa muda wa vikao vyake (3)
CAPE TOWN - Bunge la Afrika Kusini limeanza rasmi kutumia kuba kubwa lililobadilishwa matumizi yake ya awali kama ukumbi wake wa muda wa vikao vyake, ili kuhakikisha kuwa shughuli za bunge zinaendelea baada ya moto mkali kuteketeza majengo ya kihistoria ya bunge la nchi hiyo mwaka 2022.
Muundo huo mkubwa wa kuba, ulio katika eneo la bunge mjini Cape Town, utatumika kama ukumbi mkuu wa vikao vya Bunge la Kitaifa huku juhudi za ukarabati wa majengo ya awali zikiendelea, ingawa muda wa mchakato wa ujenzi huo mpya kukamilika bado haujulikani.
Idara ya Utumishi wa Umma na Miundombinu ya Afrika Kusini ilisafirisha na kujenga kuba hilo, ambalo hapo awali lilitumika kwa mazishi ya Rais wa zamani Nelson Mandela, kwa ombi la Bunge la Kitaifa ili kutumika kwa muda kwa vikao hadi ukarabati wa Bunge utakapokamilika, taarifa iliyotolewa na idara hiyo imeeleza.
"Muundo huo, ambao kwa sasa una vifaa vya dari na uimarishaji wa kimuundo, utaliwezesha Bunge hilo kufanya vikao bila kuzuiliwa katika hali zote za hewa. Aidha, utawezesha wananchi kuona shughuli za bunge ana kwa ana kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi," Waziri wa Ujenzi na Miundombinu ya Umma wa nchi hiyo, Dean Macpherson amesema katika taarifa hiyo.
Hitaji la kuwa na ukumbi wa muda wa vikao vya bunge limeibuka baada ya moto mkubwa kukumba majengo ya bunge mjini Cape Town mwezi wa Januari 2022, ukiteketeza jengo la Bunge la Kitaifa na Jengo la Bunge la Kale.
Moto huo unaodaiwa kusababishwa na mchoma moto, umesababisha Bunge hilo kukosa eneo maalum, hali iliyolazimu wabunge kutumia maeneo mbadala, ikiwemo Ukumbi wa Jiji la Cape Town, kwa matukio muhimu kama vile Hotuba Hali ya Taifa (SONA) na mijadala ya bunge.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa anatarajiwa kutoa majibu yake kuhusu mjadala na hoja za SONA baadaye wiki hii, ikiwa ni moja ya vikao vikuu vya kwanza kufanyika katika ukumbi huo wa muda.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma