Njia mpya ya treni ya mizigo inayounganisha Mji wa Chongqing wa China na Afghanistan yazinduliwa (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 11, 2025
Njia mpya ya treni ya mizigo inayounganisha Mji wa Chongqing wa China na Afghanistan yazinduliwa
Picha ikionyesha treni ya mizigo kabla ya kuondoka katika Stesheni ya Reli ya Tuanjiecun mjini Chongqing, kusini magharibi mwa China, Februari 10, 2025. (Xinhua/Tang Yi)

CHONGQING - Treni ya mizigo, iliyosheheni vifaa vya mawasiliano na bidhaa nyingine, imeondoka kutoka Mji wa Chongqing, kusini magharibi mwa China jana Jumatatu na inatarajiwa kuwasili Afghanistan baada ya siku 12 hadi 15, ikiashiria uzinduzi wa njia mpya ya moja kwa moja ya treni ya mizigo, ambayo inapitia Kazakhstan, Uzbekistan na nchi nyingine, kati ya Chongqing na Afghanistan.

Vifaa hivyo vya mawasiliano ndani ya treni hiyo, vilivyotengenezwa na kampuni ya mawasiliano ya China ZTE, vitatumika katika maendeleo ya mitandao ya mawasiliano ya nchini humo Afghanistan.

“Kupitia huduma za treni ya mizigo ya moja kwa moja, muda wa usafirishaji umepungua kwa siku tatu hadi tano ikilinganishwa na usafiri wa barabarani hapo awali, na gharama za uchukuzi zinatarajiwa kupunguzwa kwa asilimia 15 hadi 20,” amesema Liu Jianfeng anayefanya kazi ZTE.

"Kuzinduliwa kwa mafanikio kwa treni ya moja kwa moja ya mizigo kutoka Chongqing hadi Afghanistan inaonyesha juhudi nyingine katika kuzidisha ushirikiano wetu wa kiuchumi na kibiashara na nchi za Asia ya Kati," amesema Xu Runqiu, mtendaji mkuu katika kampuni ya usimamizi wa usambazaji bidhaa ya Yuxin'ou (Chongqing).

Katika miaka ya hivi karibuni, mji huo wa Chongqing umekuwa ukijitahidi kujijengea kuwa kituo jumuishi ndani ya bara, huku idadi ya treni za mizigo za kati ya China na Ulaya na zile zinazoelekea katika nchi za Asia ya Kati kutoka mji huo, pamoja na kiwango cha usafirishaji wa mizigo, vikiongezeka.

Hadi kufikia sasa, treni za mizigo zaidi ya 18,000 zinazopita zaidi ya njia 50 za kawaida zikiunganisha mji huo na nchi za Ulaya na Asia ya Kati zimeondoka mjini humo, zikifikia zaidi ya miji na maeneo 100 barani Asia na Ulaya.

Mwezi Machi 2011, huduma ya treni ya mizigo ya kati ya China na Ulaya (Yuxin'ou) ilizinduliwa kutoka Chongqing hadi Duisburg, ikianzisha njia ya moja kwa moja ya kibiashara ya nchi kavu kati ya China na Ulaya. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha