

Lugha Nyingine
Israel yaonya kuanza tena mashambulizi dhidi ya Gaza kama Hamas itashindwa kuwaachilia huru mateka ifikapo Jumamosi
![]() |
Picha hii iliyopigwa Februari 10, 2025 ikionyesha kambi ya hema kwa familia zilizokimbia makazi yao Mjini Gaza. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua) |
JERUSALEM - Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kwamba kama mateka wa Israel wanaoshikiliwa huko Gaza hawatarudishwa ifikapo Jumamosi wiki hii, makubaliano ya kusimamisha vita na Hamas yatafutwa, na Israel itaanza tena "mapigano makali" kwenye ukanda huo. Katika taarifa yake kwa njia ya video jana Jumanne, Netanyahu amesema hatua hiyo imeidhinishwa kwa kauli moja na mawaziri wake wa Baraza la Mawaziri kwenye mkutano wa saa nne uliofanyika mapema mchana.
Chini ya uamuzi huo, "kama Hamas haitawarejesha mateka wetu ifikapo saa sita mchana Jumamosi, usimamishaji vita utasitishwa, na IDF (Vikosi vya Ulinzi vya Israel) vitaanzisha tena mapigano makali hadi Hamas ishindwe kabisa," amesema.
“Mawaziri wote wa Baraza la Mawaziri la Israel wamekaribisha mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kutwaa Gaza na muda wa mwisho kusimamisha mapigano,” ameongeza waziri mkuu huyo.
Kauli hizo za Netanyahu zimekuja siku moja baada ya Hamas kutangaza kuwa makabidhiano ya mateka yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Jumamosi wiki hii yataahirishwa hadi itakapotangazwa tena.
Trump pia alitoa muda huo wa mwisho kwa Hamas siku ya Jumatatu, akisema kama mateka wote wa Israel hawatakuwa wameachiliwa huru kutoka Gaza kufikia saa sita mchana Jumamosi hiyo, atapendekeza kufuta makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano na kuacha mashambulizi yaendelee.
Hatua hizo za sasa zinakuja baada ya ujumbe wa Israel kurejea kutoka Qatar, ambako mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yamefanyika kuhusu awamu inayofuata ya makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya Israel na Hamas, na huku kukiwa na malalamiko ya kikanda na kimataifa dhidi ya kauli hizo za Trump na Netanyahu zilizotolewa hivi karibuni kuhusu Gaza.
Mapema Februari 4, Trump alitangaza mpango wenye utata wa kutwaa Ukanda wa Gaza na kuhamisha Wapalestina kutoka katika eneo hilo kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Netanyahu mjini Washington.
Siku mbili baadaye, Netanyahu alipendekeza kwenye mahojiano na Televisheni ya Channel 14 ya Israel kwamba "Wasaudi wanaweza kuanzisha taifa la Palestina nchini Saudi Arabia; wana ardhi nyingi huko."
Siku ya Jumatatu wiki hii, alipoulizwa kwenye mahojiano na Kituo cha Utangazaji cha Fox News kama Wapalestina wanaoishi Gaza sasa, ambao chini ya pendekezo la Trump watakabiliwa na kulazimishwa kuhamishwa ili kutoa nafasi ya ujenzi upya wa ukanda huo, "watakuwa na haki ya kurudi," Trump alisema, "Hapana, hawatakuwa na haki hiyo."
Zikijibu kauli hizo za Trump na Netanyahu, nchi nyingi zimeelezea kukataa kwao kuhamishwa kwa Wapalestina kutoka nchi yao na uungaji mkono wao kwa suluhu ya nchi mbili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma