Vizuizi vya muda mrefu vya kimuundo vinaifanya Afrika kuwa tegemezi kiuchumi: Mkuu wa UNECA

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 13, 2025
Vizuizi vya muda mrefu vya kimuundo vinaifanya Afrika kuwa tegemezi kiuchumi: Mkuu wa UNECA
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) Claver Gatete (wa kwanza kulia) akihutubia Mkutano wa 46 wa Kawaida wa Baraza Tendaji la Umoja wa Afrika (AU) kwenye makao makuu ya AU mjini Addis Ababa, Ethiopia, Februari 12, 2025. (Xinhua/Michael Tewelde)

ADDIS ABABA - Afrika imekuwa ikikabiliwa na vizuizi vya muda mrefu vya kimuundo ambavyo vinaziweka nchi za bara hilo katika mzunguko wa utegemezi wa kiuchumi, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) Claver Gatete amesema wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 46 wa Kawaida wa Baraza Tendaji la Umoja wa Afrika (AU) katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa jana Jumatano.

Gatete amesema hali ya kifedha ya Afrika duniani kwa sasa inadhihirisha ukosefu wa usawa unaoikabili

"Biashara ya utumwa iliyovuka Bahari ya Atlantiki na utumiaji wa kikoloni uliipokonya Afrika watu, rasilimali na heshima zake, na kuacha nyuma ukosefu wa usawa ambao unaendelea katika mifumo ya kifedha, miundo ya biashara na taasisi za usimamizi wa kimataifa hadi leo," Gatete amesema kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika.

Amesema uchimbaji wa rasilimali za Afrika bila maendeleo sawia, kutothaminiwa kwa uchumi wa Afrika katika tathmini ya mikopo ya kimataifa, na vizuizi vya kimfumo kwa biashara na uwekezaji ni dalili za dhuluma hizi za kihistoria katika zama hizi.

Gatete amesema bara hilo lina asilimia 30 ya akiba ya madini duniani, ikiwa ni pamoja na asilimia 40 ya dhahabu yake na hadi asilimia 90 ya chromium na platinamu. Amesema, hata hivyo, Afrika inachukua chini ya asilimia 3 ya biashara ya kimataifa na asilimia 1 tu ya pato la viwanda duniani.

Katibu huyo mtendaji amesema kuwa dhuluma hiyo inaenea hadi kwenye viwango vya mikopo barani Afrika, ambavyo vinatawaliwa na mashirika ya nje ambayo wakati mwingine yanafanya tathmini zisizo za haki na zenye upendeleo kwa uchumi wa Afrika.

Gatete amesema ni nchi mbili tu za Afrika -- Botswana na Mauritius -- ndizo zina tathimini ya viwango vya uwekezaji, wakati nyingine, licha ya misingi thabiti ya kiuchumi, zinaelemewa na alama zenye hatari kubwa, ambazo zinaongeza gharama za kukopa, kukandamiza uwekezaji, na kuweka uchumi wa Afrika katika mzunguko wa madeni.

Ili kukabiliana na ukosefu huo wa usawa wa kiuchumi unaokabili Bara la Afrika, Gatete ametoa wito wa kufanya mageuzi ya mfumo wa fedha duniani, kurekebisha madeni, kuanzisha wakala wa kutathimini viwango vya mikopo unaoongozwa na Afrika, kuendeleza Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika, na kuweka kipaumbele kwa kuongeza thamani ndani ya bara hilo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha