

Lugha Nyingine
Hospitali Kuu ya kwanza ya rufaa inayomilikiwa kabisa na wageni nchini China yafunguliwa mjini Tianjin
TIANJIN - Hospitali kuu ya kwanza ya rufaa inayomilikiwa kabisa na mtaji wa kigeni nchini China imefunguliwa Jumatano katika Mji wa Tianjin, kaskazini mwa China, ikionyesha maendeleo mapya kabisa kufuatia kupanuliwa kwa sera ya China ya kufungua mlango katika sekta ya huduma za afya.
Hospitali hiyo yenye vitanda 500, yenye jina la Hospitali Kuu ya Perennial ya Tianjin, inawakilisha uwekezaji wenye thamani ya Yuan takriban bilioni 1 (dola za Kimarekani takriban milioni 139.4) uliofanywa na Kampuni Binafsi Hodhi ya Perennial ya Singapore.
Hospitali hiyo inatoa huduma jumuishi za matibabu ili kukidhi mahitaji ya utambuzi na matibabu ya magonjwa ya kawaida na magumu. Pia ina idara ya kimataifa ambayo hutoa huduma maalum za afya -- ikijumuisha usimamizi wa afya na udhibiti wa magonjwa sugu.
Mwezi Septemba mwaka 2024, China ilitoa tangazo la mpango wa majaribio wa kupanua ufunguaji mlango katika sekta yake ya afya, huku mji huo wa Tianjin, kaskazini mwa China ukiteuliwa kuwa moja ya mikoa na manispaa tisa kuzindua majaribio hayo ya hospitali zinazowekezwa kabisa na mtaji wa kigeni.
Pua Seck Guan, mwenyekiti mtendaji ambaye pia ni afisa mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, amesema China imeonyesha nia thabiti na muhimu ya kufungua sekta ya matibabu na afya, ambayo inatuma ishara chanya kwa jumuiya ya kimataifa ya uwekezaji, ikitoa fursa mpya za soko na kuhimiza zaidi maendeleo anuwai ya soko la matibabu la China.
“Hospitali hiyo inalenga kuanzisha upatikanaji wa rasilimali za kiwango cha juu za matibabu za kimataifa kwa wagonjwa wa China, huku pia ikitoa njia mpya kwa wagonjwa wa kigeni wanaotafuta matibabu nchini China,” Pua ameongeza.
Tangu mwaka 2000, China imekuwa ikiruhusu kuanzishwa kwa taasisi za matibabu zinazowekezwa na mtaji wa kigeni. Baada ya miongo zaidi ya miwili, kwa sasa kuna taasisi zaidi ya 60 za matibabu zinazowekezwa kwa mtaji wa kigeni nchini humo.
Hospital hiyo Kuu ya Perennial ya Tianjin ilipokea leseni ya kwanza ya biashara kwa Hospitali Kuu ya rufaa inayomilikiwa kabisa na wageni iliyotolewa na serikali ya Mji wa Tianjin mwezi Desemba mwaka jana.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma