Kamati ya Kitaifa ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China yafanya kikao chake cha tatu cha wajumbe wote

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 10, 2025
Kamati ya Kitaifa ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China yafanya kikao chake cha tatu cha wajumbe wote
Kikao cha tatu cha wajumbe wote cha mkutano wa tatu wa Kamati ya 14 ya Kitaifa ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China (CPPCC) kikifanyika kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, Machi 9, 2025. (Xinhua/Jin Liangkuai)

BEIJING - Kamati ya 14 ya Kitaifa ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China (CPPCC), ambacho ni chombo cha juu cha mashauriano ya kisiasa cha China, jana Jumapili ilifanya kikao cha tatu cha wajumbe wote cha mkutano mkuu wa mwaka unaoendelea mjini Beijing, na Wang Huning, mjumbe wa kudumu wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China , alihudhuria kikao hicho.

Kwenye kikao hicho, washauri wa kisiasa wa kitaifa 14 wametoa maoni yao kuhusu mada mbalimbali ambapo maofisa waandamizi kutoka Kamati Kuu ya CPC na Baraza la Serikali la China walialikwa kusikiliza mapendekezo .

Mjumbe Tu Haiming, amesifu maendeleo yaliyopatikana Hong Kong, ambayo yameonesha kwa mara nyingine tena kuwa mkoa huo unaweza kutegemea taifa lake.

Amesisitiza haja ya kuwawezesha wakazi wa huko kuongeza hali ya kujiamini kitamaduni na utambuzi wa taifa lao ili kutimiza mafanikio endelevu ya utekelezaji wa sera ya "nchi moja, mifumo miwili."

Mjumbe mwingine Zhang Guanghan amehimiza kuanzishwa haraka kwa mfumo kamili wa ulinzi wa mali ya urithi wa kitamaduni, akitoa wito wa kukamilishwa kwa sheria na kanuni, kuanzisha njia mpya za usimamizi, na kufanya juhudi zaidi za kuongeza uelewa wa umma.

Ameongeza kuwa juhudi lazima zifanywe kuhakikisha jamii nzima inashiriki, kuunga mkono, na kuhimiza ulinzi wa kimfumo na usimamizi wa pamoja juu ya mali ya urithi wa kitamaduni.

Naye mjumbe Zhao Yingmin, ametoa wito wa kuchukua hatua za kuifanya mifumo na uwezo wa usimamizi wa mazingira kuwa ya kisasa.

“Kazi inahitaji kufanywa ili kuratibu kupunguza utoaji hewa ya kaboni, kupunguza uchafuzi kwa mazingira, maendeleo ya kijani, na ukuaji wa uchumi,” ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha