

Lugha Nyingine
Masoko ya mitaani yachochea tasnia ya ubunifu katika mji mkuu wa Namibia
![]() |
Mwanamume akitembelea banda kwenye soko la sanaa la mtaani mjini Windhoek, Namibia, Machi 8, 2025. (Picha na Ndalimpinga Iita/Xinhua) |
WINDHOEK - Masoko ya mitaani mjini Windhoek, mji mkuu wa Namibia, yanachochea ukuaji mkubwa katika tasnia ya ubunifu huku kukiwa na fursa finyu za kibiashara kwa wasanii wenyeji nchini humo.
Katika wilaya ya kati ya kibiashara ya Windhoek, Christina Omole amegeuza sehemu ya umma kuwa jumba la wazi la sanaa, akionyesha vito, kazi za mikono, na mavazi kwenye kibanda chake cha muda.
"Hapa ndipo sanaa ya ubunifu inapochomoza kwa maisha, ikitengeneza fursa za kijasiriamali kwa wasanii wenyeji," amesema msanii huyo mkongwe aliye katika umri wake wa miaka ya 70.
Omole amekuwa akifanya biashara katika nafasi hiyo tangu 1990, ambayo inaendelea kuwa njia yake kuu ya kupata mapato kutokana na kazi yake ya sanaa. "Kwa miaka 35, nafasi hii imekuwa njia yangu ya kutoka. Kama ningetoka, nisingejua niuze wapi kwa sababu kuna majukwaa machache ya kufanya biashara ya kazi za sanaa nchini Namibia. Kwa hivyo nabaki," ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Wakati Omole alipoanza, aliuza hasa kazi za sanaa zilizotengenezwa kwa mikono. Lakini mnyororo wa thamani wa ugavi ulibadilika kadri muda ulivyosonga. "Mwanzoni, niliofa tu vito, lakini wateja pia walitaka nakshi za mbao. Nilitengeneza mtandao wa wachongaji wenyeji," amesema.
Mzee huyo wa Namibia hayuko peke yake katika kutafuta riziki kutokana na ubunifu. Katika soko lingine lenye pilika nyingi kando ya Mtaa wa Independence, mtaa mrefu zaidi wa Windhoek, Denzel Oshondili anaendeleza desturi ya familia ya kuuza sanaa.
"Bibi yangu alianza kuuza bidhaa za sanaa mjini miaka 35 iliyopita. Sasa kwa kuwa yeye umri umeenda na anajikita katika uzalishaji, nasimamia mauzo," amesema Oshondili, ambaye ana umri wa miaka 30.
Kama ilivyo kwa Omole, baadhi ya bidhaa katika kibanda cha Oshondili zimetengenezwa nyumbani, huku nyingine zikitoka nje ya nchi. Wasanii hao wameanzisha ushirikiano na wabunifu kutoka nchi kama Botswana, Afrika Kusini, Tanzania, Kenya na Zimbabwe, ili kutoa bidhaa hitajika ambazo bado hawawezi kutengeneza wenyewe.
Mapato yanayotokana na mauzo yao yanaweza kutofautiana sana. Mapato ya siku kadhaa yanazidi dola 3,000 za Namibia (kama dola za Marekani 164), wakati mapato ya siku nyingine ni kidogo. "Lakini haijalishi ni kiasi gani, bado kinaendeleza riziki yetu," Oshondili ameongeza.
Zaidi ya faida za kifedha, wasanii hao wameanuwaisha ofa zao na kutumia mikakati mbali mbali ya uuzaji ili kuvutia wateja. Kwa Oshondili, "oda za wale wanaotaka bidhaa maalum" zimeleta mabadiliko kwa biashara yake inayostawi.
Wachuuzi pia huonyesha wateja na watalii jinsi bidhaa kama vile vito vya mapambo hutengenezwa. "Hii inawapa watalii uzoefu wa moja kwa moja wa mchakato wa uzalishaji na kuongeza uthamini wao kwa sanaa ya Namibia," Omole amesema.
Ripoti ya Takwimu ya Watalii 2023, iliyochapishwa na Wizara ya Mazingira, Misitu na Utalii ya Namibia, inaonyesha kuimarika kwa utalii baada ya kuzuka kwa COVID-19. Idadi ya watalii waliofika kimataifa iliongezeka kutoka 461,027 mwaka 2022 hadi 863,872 mwaka 2023.
Isobel Manuel, mhadhiri mkuu wa sekta ukarimu na utalii katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Namibia, amezungumzia mabadiliko kutoka kwa utalii wa kutazama tu sanaa, hali ambayo imesababisha kustawi kwa sekta ya biashara ya sanaa na ubunifu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma