

Lugha Nyingine
Abiria 21, wanajeshi 4 na magaidi 33 wauawa katika shambulizi la treni nchini Pakistan
![]() |
Abiria waliookolewa na vikosi vya usalama wakiwasili katika stesheni ya treni mjini Quetta, Jimbo la Balochistan, Pakistan, Machi 12, 2025. (Str/Xinhua) |
ISLAMABAD - Abiria 21, wanajeshi wanne na magaidi 33 wameuawa baada ya magaidi waliokuwa na silaha nzito kushambulia treni ya abiria na kushikilia mateka kadhaa katika Jimbo la Balochistan kusini magharibi mwa nchi hiyo, Idara ya Huduma za Uhusiano wa Umma (ISPR), ambayo ni tawi la vyombo vya habari vya Jeshi la Pakistan, imesema katika taarifa iliyotolewa jana Jumatano usiku.
Treni ya Huduma za Haraka ya Jaffar, iliyokuwa ikisafiri kutoka Mji wa Quetta wa jimbo hilo la Balochistan kuelekea katika mji wa Peshawar kaskazini-magharibi mwa Pakistan, ilishambuliwa siku ya Jumanne na magaidi hao karibu na wilaya ya Sibbi, ISPR imesema, ikiongeza kuwa magaidi hao, baada ya kulipua njia ya reli, walichukua udhibiti wa treni hiyo na kushikilia abiria mateka wakiwemo wanawake na watoto, wakiwatumia kama ngao za binadamu.
ISPR imesema kuwa vikosi vya usalama mara moja viliitikia hali hiyo, na kwa mafanikio kuua magaidi wote 33 wakiwemo washambuliaji wa kujitoa mhanga, huku wakiokoa mateka hao kwa awamu.
Hata hivyo, katika kipindi cha hali nzito ya sintofahamu magaidi hao waliua abiria 21 wasio na hatia kabla ya kuanza kwa operesheni ya kuwaangamiza, ISPR imesema, ikiongeza kuwa wanajeshi wanne pia wamepoteza maisha kwenye operesheni hiyo dhidi ya magaidi hao.
Operesheni ya kusafisha hali inafanywa katika eneo hilo na "waungaji mkono kitendo hicho cha woga na kiovu" watafikishwa kwenye mikono ya sheria, imesema ISPR.
Imesema kuwa shambulizi hilo limepangwa na kuongozwa na viongozi wa tawi la kigaidi linaloendesha shughuli zao kutokea Afghanistan, ambao walikuwa wakiwasiliana moja kwa moja na magaidi hao wakati wote wa tukio.
"Tunatarajia serikali ya mpito ya Afghanistan kushilikia wajibu wake na kukataa ardhi yake kutumiwa kwa shughuli za kigaidi dhidi ya Pakistan," imesema taarifa hiyo.
Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif wamelaani vikali shambulizi hilo, na kuelezea huzuni na masikitiko yao kutokana na kupoteza raia na maafisa wa usalama, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa viongozi hao wawili.
Jeshi la Ukombozi wa Balochistan ambalo limetangazwa kuwa ni kundi la kigaidi limedai kuhusika na shambulizi hilo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma