

Lugha Nyingine
Wanafunzi wa Lugha ya Kichina wa Botswana wakumbatia lugha kupitia sanaa ya KungFu
GABORONE - Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Botswana (CIUB) imeandaa shughuli ya kitamaduni na lugha iliyofanyika Ijumaa iliyopita, ikiwapa watu wanaojifunza Lugha ya Kichina jukwaa la kufanya mazoezi ya kuzungumza lugha hiyo wakati huohuo wakijenga ufahamu wa sanaa ya jadi ya KungFu ya China.
Ikiwa imefanyika chini ya kaulimbiu ya "KungFu ya China," ambayo inarejelea sanaa ya kujihami ya Kichina, shughuli hiyo imewafahamisha washiriki msamiati wa silaha za Sanaa hiyo ya Kichina, zikiwemo visu, panga, mikuki na mijeledi, sambamba na mijongeo ya msingi ya sanaa hiyo. Kipindi hicho changamani kililenga kuongeza umahiri wa kuzungumza wakati huohuo kuzidisha maelewano ya kitamaduni.
"Habari, kila mmoja. Jina langu ni Shen Chenggong," alisema Keagile Sebetlela, mwanafunzi wa CIUB, alipokuwa akijitambulisha kwa Lugha ya Kichina kwenye mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua katika hafla hiyo.
"Nina nia ya kujifunza lugha ya Kichina kwa sababu, kwa maoni yangu, imekuwa moja ya lugha kuu za kimataifa. Ninaamini kujua lugha ya Kichina kunaweza kufungua milango mingi," amesema Sebetlela, akiongeza kuwa anapenda sana kuandika maandishi ya Kichina, kwani lugha hiyo hutofautiana na zingine nyingi zinazotegemea alfabeti.
Wanafunzi Sharon Khumotse na Lindiwe Lile Ramooki walitumbuiza katika hafla hiyo, wakijitambulisha kwa majina yao ya Kichina kabla ya kutoa maonyesho kwa wahudhuriaji kwa kutumia maneno magumu ya kutamkwa kwa haraka mfululizo.
"Mimi ni mwanafunzi wa lugha ya Kichina nimekuwa nikisoma lugha hiyo kwa miaka mitatu. Ninafanya kazi katika ofisi ya benki," Ramooki alisema kwa lugha fasaha ya Kichina.
Kwa Fidelity Monthe, anayejulikana kwa jina la Kichina la Fei Di'an, kujifunza lugha hiyo ni muhimu ili kukuza biashara yake.
"Ninafanya biashara ndogo ndogo na nimekuwa nikisafiri kwenda China kutafuta bidhaa. Changamoto kubwa imekuwa mawasiliano. Kujifunza lugha ya Kichina kutanisaidia kupanua biashara yangu na kujenga ushirikiano na kampuni za China," Monthe ameliambia Xinhua.
Monthe na Sebetlela ni miongoni mwa wanafunzi na walimu wapatao 70 wa lugha Kichina walioshiriki katika shughuli hiyo ya saa mbili, ambayo ilijumuisha maonyesho ya nyimbo za Kichina, michezo ya lugha, na mijadala ya vikundi.
Pu Durong, mkurugenzi wa China wa CIUB, amefananisha shughuli hiyo na "kona za Kiingereza" nchini China, ambapo wanafunzi wa lugha hukusanyika ili kufanya mazoezi ya kuzungumza.
"Nchini China, tuna kona za Kiingereza kwa ajili ya kufanya mazoezi ya Kiingereza. Hapa Botswana, tuna kona ya Kichina kwa wanafunzi kuboresha ujuzi wao wa kuzungumza. Wanafunzi hawa wanapenda sana lugha, kwa sababu wengi wanapanga kufanya biashara nchini China," Pu amesema.
CIUB, Taasisi ya kwanza ya Confucius nchini Botswana, ilifuatiwa na taasisi ya pili iliyozinduliwa Oktoba 2023, katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Sayansi na Teknolojia cha Botswana mjini Palapye, yapata umbali wa kilomita 270 kaskazini mashariki mwa Gaborone, mji mkuu wa nchi hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma