

Lugha Nyingine
Watu takriban 6 wafariki na wengine 9 kujeruhiwa baada ya manowari ya kitalii kuzama katika Bahari Nyekundu nchini Misri
![]() |
Picha hii iliyopigwa tarehe 27 Machi 2025 ikionyesha eneo la uokoaji kwa ajili ya manowari ya kitalii iliyozama kwenye Bahari Nyekundu karibu na pwani ya Hurghada, Misri. (Picha na Ali Awad/Xinhua) |
CAIRO – Watu takriban sita wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa siku ya Alhamisi wakati manowari ya kitalii ilipozama kwenye Bahari Nyekundu nchini Misri katika safari ya kitalii kwenye mji wa mapumziko wa Hurghada, chanzo rasmi cha habari katika Jimbo la Bahari Nyekundu kimeliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Watano kati ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya, huku abiria wengine 29 wakiwa wameokolewa na kurudishwa kwenye hoteli zao, kwa mujibu wa chanzo hicho ambacho kilizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Kimeongeza kuwa sababu ya tukio hilo bado inachunguzwa, na uraia wa waathiriwa hao bado haujajulikana.
Kwa mujibu wa baadhi ya vyombo vya habari vya Misri, kikiwemo kile kinachosomwa kwa wingi cha tovuti ya Al-Masry Al-Youm, manowari hiyo ya kitalii, yenye jina la Sindbad, ilikuwa imebeba abiria 44 kwenye safari hiyo ya kutalii chini ya maji kujionea miamba ya matumbawe.
Wakati huo huo, chombo cha habari cha serikali ya Russia, RIA Novosti kimenukuu taarifa kutoka Ubalozi mdogo wa Russia katika mji huo wa Hurghada ikionesha kwamba watalii wote waliokuwa ndani ya manowari hiyo ni raia wa Russia.
"Kulikuwa na watalii 45 ndani yake, wakiwemo watoto wadogo, vilevile wafanyakazi. Wote ni raia wa Russia, watalii wa kampuni ya Biblio Globus," taarifa hiyo imesema, ikinukuliwa na RIA Novosti.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma