

Lugha Nyingine
Iran yasema urutubishaji wa uranium, unafuu wa vikwazo ni matakwa yasiyo ya mjadala katika mazungumzo na Marekani (3)
![]() |
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei akihudhuria mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, tarehe 28 Aprili 2025. (Xinhua/Shadati) |
TEHRAN - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei kwenye mkutano na waandishi wa habari wa kila wiki jana Jumatatu mjini Tehran wakati akifafanua juu ya matakwa ya nchi hiyo kwenye mazungumzo na Marekani ya upatanishi wa Oman amesema kwamba urutubishaji wa ndani wa madini ya uranium na uondoaji kikamilifu vikwazo ni matakwa yasiyo ya mjadala ya Tehran katika majadiliano hayo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea Washington.
Duru tatu za majadiliano hayo zimeshafanyika hadi sasa, mbili katika mji mkuu wa Oman, Muscat Aprili 12 na Aprili 26, mtawaliwa, na nyingine mjini Roma, Italia Aprili 19.
Baghaei amesema maelezo ya kina ya mazungumzo yoyote yanapaswa kuwa ndani ya mfumokazi wa majumuisho ya jumla ambao tayari umekubaliwa na pande hizo mbili, akiongeza, "Hivyo, hakuna makubaliano yatakayofikiwa isipokuwa pale mfumokazi wa jumla unaotakiwa wa Iran utakapozingatiwa."
Baghaei amesisitiza kuwa mashauriano ya kiufundi yatafanyika kwa wakati mmoja katika kila hatua ya majadiliano.
Vile vile amesisitiza kuwa "kukomesha vikwazo kikamilifu ni neno muhimu" na kwamba kuwa na ufikiaji wa mali ya Iran iliyoshikiliwa "kinyume cha sheria na bila haki" ni miongoni mwa matakwa makubwa ya nchi yake katika mazungumzo hayo.
Baghaei amebainisha kuwa ujumbe wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki uliwasili Tehran mapema siku hiyo ya jana Jumatatu kwa mazungumzo ya kiufundi na wataalamu wa Iran kuhusu mada kadhaa, ikiwemo masuala ya kulinda nyuklia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma