Rais Xi akagua jukwaa la kuzalisha modeli kubwa la Shanghai, akisisitiza matarajio ya China juu ya AI (5)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 30, 2025
Rais Xi akagua jukwaa la kuzalisha modeli kubwa la Shanghai, akisisitiza matarajio ya China juu ya AI
Rais Xi Jinping wa China, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC), akitembelea duka la kupata uzoefu wa bidhaa za AI kwenye Kituo cha Uvumbuzi wa modeli kubwa cha Shanghai Foundation, jukwaa la kuzalisha modeli kubwa ambalo limevutia kampuni zaidi ya 100 huko Shanghai, mashariki mwa China, Aprili 29, 2025. (Xinhua/Xie Huanchi)

SHANGHAI - Rais Xi Jinping wa China ametembelea Kituo cha Uvumbuzi wa modeli kubwa cha Shanghai Foundation, jukwaa la kuzalisha modeli kubwa ambalo limevutia kampuni zaidi ya 100 huko Shanghai, akihimiza mji huo kuchukua nafasi ya uongozi katika maendeleo na usimamizi wa AI huku akisisitiza uwezo mkubwa wa China katika sekta hiyo.

Ziara hiyo imekuja siku nne baada ya uongozi wa China kuitisha kikao maalumu ya kujifunza kuhusu AI, ambapo Rais Xi alitoa wito wa kupata mwanzo wa kiuongozi kwa sekta hiyo ya kimkakati.

"Teknolojia ya AI inabadilika kwa kasi kubwa na kuingia kipindi cha ukuaji mkubwa," amesema Rais Xi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC).

Wakati wa kikao hicho cha Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya CPC Ijumaa wiki iliyopita, Rais Xi alisema AI, kama teknolojia ya kimkakati inayoongoza duru mpya ya mapinduzi ya kisayansi na mageuzi ya kiviwanda, imebadilisha sana namna watu wanavyofanya kazi na kuishi.

“Kamati Kuu ya Chama inaweka umuhimu mkubwa kwenye maendeleo ya AI, na imeboresha muundo wa ngazi ya juu na kuimarisha juhudi za utekelezaji katika miaka ya hivi karibuni,” Rais Xi alisema kwenye mkutano huo.

Kwenye ziara yake hiyo katika jukwaa hilo, Rais Xi alijiunga na kongamano yenye kauli mbiu ya mapinduzi ya vyombo vinavyojiendesha vya akili bandia vya kizazi kipya, akishiriki katika majadiliano na vijana papo hapo.

"AI ni viwanda vipya, na pia ni viwanda ambavyo ni vya vijana," amesema Xi.

Kisha akaingia kwenye duka la kupata uzoefu wa bidhaa za AI, ambako aliuliza kwa kina kuhusu kazi na mwenendo wa soko la bidhaa, na akajaribu kuvaa jozi ya miwani ya akili bandia kwa kujionea inavyofanya kazi moja kwa moja.

Shanghai ilitangaza mpango wa kina Desemba mwaka jana wenye lengo la kuendeleza mfumo wa ikolojia ya sekta ya AI wa kiwango cha kimataifa ifikapo mwaka 2025, ikijumuisha hatua za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa. Mwaka 2024, kiwango cha thamani ya sekta ya AI ya Shanghai kilizidi yuan bilioni 400 (dola Kimarekani kama bilioni 55).

Soko la AI la China linakadiriwa kupata ukuaji mkubwa katika miaka ijayo, kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Data. Kampuni za Marekani, zikiwemo Tesla na Microsoft, zimeweka macho yao juu ya matarajio ya kibiashara ya soko la AI la China.

Eneo la Delta la Mto Yangtze, linalobebwa na mji wa Shanghai, liko mstari wa mbele katika uvumbuzi wa AI wa China. Programu ya AI ya DeepSeek, inayotoka Hangzhou katika sehemu ya kusini ya eneo hilo, iko umbali wa chini ya kilomita 200 kutoka Shanghai.

Akitaja rasilimali nyingi za data za China, mfumo kamili wa kiviwanda na soko kubwa, Rais Xi amesema kuwa nchi hiyo ina mustakabali mkubwa wa maendeleo ya AI, akisisitiza kuimarishwa kwa uungaji mkono wa sera na nguvu za kuandaa watu wenye ujuzi.

Rais Xi siku hiyo ya Jumanne ameihimiza Shanghai kukumbatia jukumu lake la kihistoria kama kituo ongozi cha kimataifa cha uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia na kujijengea kuwa kituo cha hali ya juu cha kisayansi na kiteknolojia unaojulikana duniani kote.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha